Uko hapa: NyumbaniHabari2021 07 11Article 546457

Habari Kuu of Sunday, 11 July 2021

Chanzo: www.habarileo.co.tz

Wadau wa elimu Z’bar wataka Kiingereza kuanzia msingi

Wadau wa elimu Z’bar wataka Kiingereza kuanzia msingi Wadau wa elimu Z’bar wataka Kiingereza kuanzia msingi

WADAU wa elimu Zanzibar wameishauri serikali iangalie uwezekano wa kuanzisha mfumo wa kutumia lugha ya Kiingereza kufundishia kuanzia shule za msingi ili kuwajengea uwezo wanafunzi katika ngazi za elimu zinazofuata.

Pia, wameshauri mtaala wa elimu ya sekondari uzingatie kutoa zaidi elimu ya ufundi na ujasiriamali badala ya kutoa kipaumbele katika masomo yanayowabana kuendelea na kidato cha tano na sita kama vile fizikia, hesabu na Kiingereza.

Wadau hao walitoa maoni hayo Zanzibar jana katika mkutano wa kupokea maoni ya wadau kuhusu uboreshaji mitaala ya elimu ya sekondari.

Mwalimu Mkuu katika moja ya shule binafsi Zanzibar, Protus Nicodem alisema lugha ya kufundishia ni tatizo kwani watoto wote wanaanza shule ya msingi katika shule za serikali kwa kutumia lugha ya Kiswahili kwa miaka saba kama lugha ya kufundishiwa.

“Unakuta mtoto huyu anapoanza kidato cha kwanza anajifunza Kiingereza atembee nacho. Kwa kweli walimu tuna kazi sana. Kama Kiingereza ndio lugha ya kufundishia sekondari, basi kianze kufundishia kuanzia shule ya msingi maana mtu anachoanza nacho ndio kizuri,” alisema.

Pia alishauri uwezo wa mtoto uangaliwe katika fani mbalimbali na kuendelezwa tofauti na sasa ambapo wanafunzi hulazimika kuingia kwenye makundi mawili ya sanaa au sayansi.

Mtumishi Chuo Kikuu cha Zanzibar, Ali Shauri Jecha alishauri kuondolewa makundi ya sanaa na sayansi na kutengenezwa makundi ya ufundi na ujasiriamali na ndio yapewe kipaumbele kuliko masomo mengine.

“Masomo ya Kiswahili, fizikia na hesabu yasimnyime mtu kuendelea na masomo, wapo wanaoshindwa kuendelea kidato cha sita kwa kushindwa masomo hayo,” alisema.

Abdultif Twalib Hamis kutoka Taasisi ya Vijana alishauri Wizara ya Elimu ifikirie kuongeza somo la ujasiriamali ili kuwawezesha walioshindwa kuendelea kidato cha sita kuongeza ujuzi mwingine wa kujiajiri.

Awali, akifungua mkutano huo, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako alisema mabadiliko ya mtaala huo ni ya sita na yamelenga kuhakikisha mitaala inaendana na hali ya jamii, siasa, uchumi, sayansi na teknolojia katika nchi na dunia kwa ujumla.

“Naomba mtoe maoni yatakayohakikisha Tanzania inakuwa na mhitimu ambaye ameiva sawasawa, mhitimu wa ndoto ya Watanzania. Dunia inashuhudia mapinduzi makubwa ya sayansi na teknolojia yaliyoleta utandawazi ambayo moja ya athari ni kuongezeka kwa ushindani katika soko la ajira,” alisema.

Profesa Ndalichako alisema katika muktadha huo kuna umuhimu mkubwa wa kuhakikisha wahitimu wanapata ujuzi na maarifa yatakayowawezesha kushindana kwa ufanisi katika soko la ajira.