Uko hapa: NyumbaniHabari2021 08 23Article 553165

Uhalifu & Adhabu of Monday, 23 August 2021

Chanzo: ippmedia.com

Wahamiaji haramu wanaswa kwenye gari lililobeba kabichi

Wahamiaji haramu wanaswa kwenye gari lililobeba kabichi Wahamiaji haramu wanaswa kwenye gari lililobeba kabichi

WAHAMIAJI haramu 38 raia wa Ethiopia wamekamatwa na Idara ya Uhamiaji wilayani Handeni mkoani Tanga, wakiwa wamejificha ndani ya gari lililobeba kabichi wakielekea Afrika Kusini.

Ofisa Uhamiaji wilayani Handeni, Joan Ndumbati, amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema kuwa, lilitokea Agosti 19, mwaka huu.

Ndumbati alisema awali walipata taarifa kutoka kwa wananchi kuhusiana na kuwapo gari la mizigo pembeni ya barabara ya shule, kuna watu wanashuka na hawaelewi wanatokea wapi na lengo lao ni nini.

Alisema askari wa uhamiaji kwa kushirikiana na viongozi wa kijiji na Kata ya Komkonga walifika eneo la tukio na kubaini uwapo wa raia hao wa Ethiopia, ambao idadi yao ilikuwa ni 50, lakini waliokamatwa ni 38 huku wengine 12 wakikimbilia katika shamba la katani lililokuwapo kwenye eneo hilo.

"Katika mahojiano na raia hao mmoja anaweza kuongea Kiswahili na kueleza kuwa wapo 50 wanatoka Ethiopia na kuelekea Afrika Kusini, ila tumebaini 12 wametoroka na kuingia kwenye shamba la katani la eneo hilo na juhudi za kuwatafuta na kuwakamata ili kufikishwa kwenye vyombo vingine vya kisheria zinaendelea," alisema Ndumbati.

Mkuu wa Wilaya ya Handeni, Siriel Mchembe, alisema kwa mwaka mmoja sasa raia wa kigeni 110 wamekamatwa kwenye vizuizi mbalimbali vya barabarani wilayani humo, awali walikamatwa 72 na leo 38 huku wengine 12 wakiendelea kutafutwa baada ya kutoroka.

Mchembe aliongeza kuwa haipendezi viongozi kukosa taarifa muhimu kama hizo, hata kama ni raia wametoa taarifa ila ilipaswa ngazi husika kwenye vizuizi ndiyo wakamate watu hao, siyo mpaka gari liharibike au kuisha mafuta.