Uko hapa: NyumbaniHabari2021 08 25Article 553531

Habari za Afya of Wednesday, 25 August 2021

Chanzo: www.habarileo.co.tz

Wajawazito bado wanadaiwa fedha huduma za afya nchini

Wajawazito bado wanadaiwa fedha huduma za afya Wajawazito bado wanadaiwa fedha huduma za afya

MADIWANI wa Halmashauri ya Mji wa Bunda mkoani Mara, wamesema licha ya Sera ya Taifa ya Afya kutaka huduma za afya ya uzazi kwa wajawazito na watoto chini ya miaka mitano zitolewe bure, bado wajawazito wanatakiwa kulipia katika vituo vya afya.

Walisema hayo juzi katika Mkutano wa Mwaka wa Fedha wa 2021/2022 wa Baraza la Madiwani uliofanyika mjini Bunda.

Diwani wa Kata ya Bunda Stoo, Flavian Nyamageko, alisema: "Sera ya serikali inasema akimama wajawazito pamoja na watoto wenye umri wa chini ya miaka mitano watibiwe bure sasa je, mwenyekiti mimi ninataka kujua mbona wanapokwenda kwenye vituo vya kutolea huduma za afya wamekuwa wakiambiwa walipie au wakanunue dawa hili likoje?"

Diwani wa Kata ya Nyamakokoto, Emmanuel Malibwa yeye alihoji akisema: "Mimi ni mmoja wa waathirika, mke wangu alikwenda hospitali akaambiwa atoe pesa, mpaka tulipotoa pesa ndipo akapewa huduma, hii sera ya serikali mbona haifuatwi?"

Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Mji wa Bunda, Dk Richard Majahasi, alisema changamoto inayoyakumba makundi hayo, inatokana na wakati mwingine waathirika kukuta vifaa tiba na dawa zikiwa zimekwisha.

Alisema kuisha kwa dawa na vifaatiba hivyo huwafanya walazimike kununua katika maduka ya serikali yaliyoko katika vituo husika kwa bei nafuu.

Hata hivyo madiwani hao walisema ni jukumu la Bohari ya Dawa (MSD) kupeleka dawa za kutosha katika vituo vya kutolea huduma za afya kwani changamoto hiyo inachonganisha serikali na wananchi.

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Bunda, Emmanuel Mkongo, alisema suala hilo ni nyeti na wamelichukua ili kulifanyia kazi na kuhakikisha wanaondoa changamoto hiyo.

Wakati huo huo: Jokofu la kuhifadhia maiti limefungwa katika Kituo cha Afya Bunda Mjini.

Kwa mujibu wa taarifa zilizopatikana, madiwani wa halmashauri hiyo wamepanga gharama za kulipia kwa maiti moja kwa siku kuwa Sh 20,000.

Jokofu hilo lilifungwa baada ya Mkuu wa Mkoa Mara, Ali Hapi, kutoa muda wa wiki moja liwe limefungwa.

Hapi alifikia hatua hiyo baada ya mwananchi mmoja ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati ya Afya katika Kituo cha Afya cha Bunda Mjini, Franco Nyamageko, kulalamika kwamba tangu liletwe na MSD zaidi ya miezi sita, halijafungwa kwenye chumba cha kuhifadhia maiti.

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji wa Bunda, Michael Kweka, aliwaomba madiwani kumpa ushirikiano wa kutosha mkurugenzi huyo mpya, ili halmashauri hiyo iweze kufanikiwa zaidi na kusonga mbele kimaendeleo