Uko hapa: NyumbaniHabari2021 08 13Article 551275

Habari za Afya of Friday, 13 August 2021

Chanzo: www.habarileo.co.tz

Wakazi DAR kupata chanjo bila masharti

Wakazi DAR kupata chanjo bila masharti Wakazi DAR kupata chanjo bila masharti

BAADHI ya vituo vya utoaji chanjo ya Covid- 19 katika Mkoa wa Dar es Salaam, vimetangaza kuanza rasmi kutoa chanjo hiyo kwa watu wote walio na umri wa miaka zaidi ya 18.

Hiyo inatokana na wito wa serikali kuwa wananchi wote wanaofika vituoni kuomba kupewa chanjo wasinyimwe.

Hivi karibuni Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Profesa Abel Makubi aliruhusu vituo vinavyotoa huduma ya chanjo ya Covid- 19 kuanza kutoa huduma hiyo kwa wananchi wenye zaidi ya miaka 18 wanaofika vituoni kuomba huduma hiyo akisema jambo la kuzingatia ni kuwatanguliza wazee na kila mmoja apate chanjo kwa hiari yake.

Moja ya vituo vilivyoitikia wito huo ni pamoja na Kituo cha Hospitali ya Shree Hindu Mandal ambacho kupitia taarifa yake iliyotolewa jana na Katibu Mkuu wake Mitesh Govindji, kilisema wananchi wote walio na miaka zaidi ya 18 wanaotaka kupata chanjo hiyo kwa hiari yao kwanza wajisajili katika tovuti ya https://chanjocovid.moh.go.tz.

Taarifa hiyo ilisema baada ya kujisajili wananchi wanapaswa kuja katika kituo hicho katika ukumbi wa Shree Sorathia Prajapati katika Mtaa wa India wakiwa na ujumbe mfupi wa kuthibitisha usajili huo pamoja na kitambulisho cha taifa au pasi ya kusafiria.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, kwa wananchi wasiokuwa na uwezo wa kuingia katika mtandao na kupata huduma hiyo, wanatakiwa kufika katika kituo hicho wakiwa na kitambulisho cha taifa au pasi ya kusafiria wataelezwa taratibu za kufanya ili waweze kupata chanjo hiyo.

Taarifa hiyo ilisema baada ya kupata chanjo hiyo serikali itatoa cheti cha mtandao kuthibitisha chanjo hiyo kulingana na upatikanaji wake. Kituo kitafunguliwa kuanzia Jumatatu hadi Jumamosi saa tatu asubuhi hadi saa tisa alasiri.