Uko hapa: NyumbaniHabari2021 08 30Article 554503

Habari za Afya of Monday, 30 August 2021

Chanzo: MWANANCHI

Wakuu taasisi za dini nchini wameunda kikosi kazi cha chanjo ya COVID-19

Chanjo ya UVIKO-19 Chanjo ya UVIKO-19

Viongozi wakuu wa taasisi za dini nchini wameunda kikosi kazi kwa ajili ya kushughulikia masuala yahusuyo Uviko-19 (Religious Leader Task Force) ili kutoa elimu jinsi ya kukabiliana na maambukizi hayo wakati wa kuabudu na kubadilisha mitazamo, fikira, mila na desturi kuhusu chanjo ya ugonjwa huo.

Kikosi kazi hiko kimeundwa na viongozi wa taasisi za dini kutoka Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA) na Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT) na kuunda hadidu za rejea 23 zitakazowapa miongozo katika utekelezaji wao.

Akizungumza katika kikao cha kutoa elimu kwa viongozi wa dini kuhusu Uviko-19 Mkoa wa Dodoma leo Jumatatu Agosti 30, 2021 Nosim Peter kutoka idara ya afya KKKT makao makuu Arusha alisema lengo la kuanzisha semina hizo ni kuondoa mtazamo hasi juu ya chanjo ya Uviko-19, hivyo kupitia viongozi wa dini suala hilo litakuwa jepesi kwani wana watu wengi wanaowaamini na kuwasikiliza.

Amesema kwa sasa wametembelea mkoa wa Arusha, Kilimanjaro na Rukwa huku wakiwa wana mpango wa kuifikia mikoa yote ambayo imeathiriwa zaidi na muingiliano wa watu ukiwemo Dar es Salaam.

“Tumeandaa mkutano huu kwasababu tunajua viongozi wa dini wana watu ambao wanapatikana makanisani na misikitini kwa kujua nguvu hiyo tukaona ni vema kuwajengea wao uwezo wa kuelewa na kusaidia upatikanaji wa elimu kuhusu Uviko- 19 na kuangalia usalama wa ibada mbalimbali ambazo zinafanyika”amesema

Kwa upande wake mshauri wa kikosi kazi cha madhehebu mbalimbali kuhusu Uviko- 19, Dk Paul Kisanga alisema lengo la kikosi kazi hicho ni kuweka njia salama ambazo zitasaidia waumini kufanya ibada zao kwa kutumia tahadhari ya kueneza maambukizi ya Uviko-19.

Dk Paul amesema wananchi waache kufuata maneno ya mitandaoni kuhusu chanjo likiwemo ugandaji wa damu na badala yake kuwasikiliza viongozi wa afya kwani chanjo ina maudhi madogo madogo kwa baadhi ya watu hivyo ni kawaida.

“Kuna uwezekano wa watu kuwa na matatizo yao tofauti na chanjo ndo vikaingiliana, damu haiwezi kuganda dakika hiyo hiyo haijawahi kutokea, sasahivi Marekani wameshachanja watu zaidi ya 15 milioni kwa chanjo ya JJ na hadi kufikia Februari watu 7 milioni kati ya hao waliochanja, watu 6 tu walionekana kuganda kwa damu."