Uko hapa: NyumbaniHabari2021 09 24Article 559561

Habari za Afya of Friday, 24 September 2021

Chanzo: www.habarileo.co.tz

"Waliochanja wapo salama kwa 85% - JKCI Hospital

"Waliochanja wapo salama kwa 85% - JKCI Hospital

KAIMU Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dk. Tatizo Waane, amesema mtu anapopata chanjo ya Corona anakua kwenye nafasi ndogo ya kupata changamoto kubwa za kiafya kwa asilimia 85.

Waane ameyasema hayo leo wakati wataalam wa afya kutoka Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) walipoalikwa na uongozi wa Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) kwa ajili ya kutoa elimu ya umuhimu wa chanjo pamoja na kutoa chanjo ya Corona kwa wafanyakazi wa benki hiyo Jijini Dar es Salaam

Amesema watu wengi waliopata ugonjwa wa Corona asilimia 85 walipata maradhi madogo madogo kama vile kuumwa kichwa, mafua na homa za hapa na pale, asilimia 10 walifikia hatua za kupata huduma za hospitali kama vile kulazwa na kadhalika, lakini asilimia tano walifikia hatua za kutumia msaada wa mashine kupumua.

“Kama leo wote tutachanja ni matumaini yangu hata ikitokea tukapata ugonjwa huu tutaishia kwenye ile asilimia 85 ya kusumbuliwa na maradhi madogo madogo”, amesema Dk Waane

Kwa upande wa Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Dk Rashid Mfaume, amesema serikali imeandaa mpango wa jamii shirikishi na harakishi wa utoaji wa chanjo dhidi ya ugonjwa wa Corona kwa kuwafuata wananchi wanaohitaji huduma ya chanjo mahali walipo ili kuongeza kasi na kuwapa wananchi nafasi ya kuchanja.

Dk Mfaume amesema kitendo kilichofanywa na JKCI kwa kushirikiana na TADB ni maelekezo ya Serikali kwamba lazima sasa wataalam wa afya watoke na kuwafuata wananchi wenye uhitaji wa chanjo ya Corona pale walipo.

“Wafanyakazi hawawezi wakafanya kazi wasipokuwa na afya njema, maamuzi mliyoyafanya ya kupata chanjo kwa namna moja ama nyingine mtakuwa mnatekeleza sera zenu”, alisema Dk. Mfaume.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) Frank Nyabundege amesema menejimenti ya Benki yake imeona ni vyema kuwapa nafasi wafanyakazi wa benki hiyo ili waweze kupata elimu juu ya ugonjwa wa Corona pamoja na chanjo, kwani kupitia elimu sahihi waliyoipata wengi wao watabadili mawazo potofu waliyokuwa nayo.