Uko hapa: NyumbaniHabari2022 01 11Article 585046

Habari za Mikoani of Tuesday, 11 January 2022

Chanzo: www.tanzaniaweb.com

Waliohitimu la saba wote kuendelea na masomo Mbeya

Waliohitimu la saba wote kuendelea na masomo Mbeya Waliohitimu la saba wote kuendelea na masomo Mbeya

Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Juma Homera amesema hawatarajii kuona mtoto yeyote akizurura shule zitakapofunguliwa kwani hata ambao hawakufaulu kuendelea na sekondari wametengewa vyuo vya ufundi (Veta) ndani na nje ya Mkoa huo, huku akizitaka Halmashauri zote kutenga bajeti kwa ajili ya ujenzi wa shule moja moja ya mchepuo wa kiingereza.

Shule za msingi na sekondari zinatarajiwa kufunguliwa Januari 17, ambapo zaidi ya wanafunzi 39,000 waliofaulu wanatarajia kuanza kidato cha kwanza kwa mwaka huu 2022 mkoani hapa. Akizungumza wakati wa kukabidhiwa madarasa 84 yaliyojengwa kwa mradi wa fedha za Uviko-19, Homera amesema mwaka huu shule zitakapofunguliwa hawatarajii kuona mtoto yeyote akizurura mitaani.

Amesema wanafunzi 39,000 wanatarajia kuanza masomo ya sekondari kidato cha kwanza, huku wengine takribani 5,000 wakipelekwa kwenye vyuo vya ufundi (Veta) ndani na nje ya Mkoa. "Hadi sasa madarasa yako tayari yakisubiri wanafunzi tofauti na miaka mingine nyuma, ambapo mwanafunzi alikuwa anasubiri darasa lijengwe, inamaana mwaka huu hakutakuwa na mtoto wa kazi za nyumbani, bodaboda au kuzurura mitaani kwani hata ambao hawakufaulu kuendelea na kidato cha kwanza, watapelekwa Veta" amesema Homera.

Mkuu huyo pia amemuagiza Katibu Tawala Mkoa, Angelina Lutambi kuziandikia barua halmashauri zote za Mkoa huo kuhakikisha zinajenga shule moja ya msingi ya mchepuo wa kiingereza ili kuongeza zaidi ufaulu akidai kuwa zilizopo kwa sasa hazitoshi na watoto wanakosa haki yao.

Amesema kwa sasa Mkoa huo una shule tano za mchepuo wa kiingereza, ikiwa ni Shule ya Msingi Mkapa, Azimio, Magufuli, Kambarage na Chief Mwashinga na kwamba idadi hiyo haitoshi na kuzitaka Halmashauri kutenga bajeti kwa ajili ya kujenga shule moja kila eneo.

"RAS nakuagiza ziandikie barua Halmashauri zote kuhakikisha wanatenga bajeti ya kujenga shule moja ya Msingi yenye mchepuo wa kiingereza ili kuwapa nafasi watoto kupata Elimu na kuboresha zaidi kiwango cha ufaulu" amesema Mkuu huyo.

Hata hivyo Homera ameonesha kufurahishwa na matokeo ya darasa la saba, akisema wakati anawasili Mbeya, Mkoa huo ulikuwa nafasi ya 13, lakini matokeo ya mwaka jana wameshika nafasi ya tatu kwa ufaulu kitaifa na kwamba wanataka matokeo ya mwaka huu washike namba moja.

Kwa upande wake Meya wa Jiji la Mbeya, Doromohamed Issa amesema kutokana na fedha walizotengewa na serikali chini ya Rais, Samia Suluhu Hassan wanaamini kufikia 2030, Mkoa wa Mbeya utakuwa kama Jiji la Toronto kwani bajeti inagusa maeneo yote ya huduma za jamii na kuwaomba wananchi kuendelea kuiamini na serikali na kuwaombea viongozi.

"Shule zinaendelea kujengwa, vituo vya afya, zahanati, hospitali, barabara, maji na nishati kila upande Rais wetu ametugusa, mimi naamini kufikia 2030, Mbeya itakuwa Toronto" amesema Issa.

Naye Jawila Hassan mmoja wa wazazi katika shule ya Sekondari Ihanga amesema uwepo wa madarasa na madawati itasaidia watoto wao kusoma katika mazingira mazuri na kuongeza ufaulu.

"Zamani michango ilikuwa mingi, lakini kwa sasa tunashukuru kuona watoto wetu wanasomea kwenye gholofa na madawati yapo, enzi zetu ilikuwa vichekesho ilikuwa kwenye miti na vumbi tu" amesema Jawila.