Uko hapa: NyumbaniHabari2021 05 28Article 540286

Habari za Mikoani of Friday, 28 May 2021

Chanzo: www.habarileo.co.tz

Wamanda na ngoma yao ya mganda

Wamanda na ngoma yao ya mganda Wamanda na ngoma yao ya mganda

MILA au utamaduni ni namna watu wanavyofanya mambo yao kwa kawaida kama vile; wakati gani au nini wanakula, mavazi yao, wanasalimiana vipi, mambo ambayo ni adabu, miiko yao, mambo wanayoamini n.k.

Mambo ambayo yanaweza kuutambulisha utamaduni wa watu wa jamii fulani ni mengi na anwai.

Leo katika mwendelezo wa makala za utamaduni, mila na desturi za makabila mbalimbali ya Tanzania, tunaangazia jamii ya Wamanda.

Wamanda ni kabila la watu wanaoishi katika mwambao wa Ziwa Nyasa wilayani Ludewa katika Mkoa wa Njombe. Mbali na Wamanda, Wilaya ya Ludewa ina makabila mengine ya Wapangwa na Wakisi, kabila ambalo linapatikana pembezoni mwa Ziwa Nyasa.

Wamanda wanapatikana zaidi katika Kata za Manda, Ruhuhu, Luilo, Iwela, Mkomang’ombe, Ludewa na Masasi.

Vijiji maarufu vya Manda ni pamoja na Igalu, Ilela (Ilela ilihama kutoka ziwani; zamani hiyo sehemu ilikuwa ndiyo Ngelenge), Luilo, Mbongo, Masasi, Ngelenge (Ngelenge zamani ilikuwa inatiwa Kulondoni; kwa sasa Ngelenge inaunganisha vijiji vya zamani vya Kuliwolelo, Kuntudu, Kupanda, Kutakanini na Kulondoni), Kumasasi, Nsungu, Kipingo na Lihanguli.

Wamanda pia wanapatikana katika Wilaya za Mbinga na Nyasa mkoani

Ruvuma, hasa eneo la kaskazini mwa wilaya hizo, na baadhi ya Wamanda wanaishi katika maeneo ya Gua na Mkwajuni katika Wilaya ya Chunya mkoani Mbeya.

Kwa ufupi, Wamanda wanapatikana zaidi katika Wilaya za Ludewa, Mbinga na Nyasa kuanzia eneo la Lituhi, Ndongosi na kata za jirani upande wa Wilaya ya Nyasa.

Wamanda wa Ndongosi wengi wao walihamia eneo hilo wakitokea eneo la Lituhi na vijiji vya karibu kama Kunkaya, Kumangori n.k. kutokana na kiongozi mmoja wa serikali kuundanganya uongozi wa juu wa serikali kwa manufaa yake, kwa kudai kuwa eneo lote la Lituhi lipo majini.

Mila na desturi za Wamanda

Kwa mujibu wa wenyeji wa Wilaya ya Ludewa, inasemwa kuwa, wilaya hiyo ina tamaduni zake, mila na desturi zikiwemo ngoma za kiutamaduni na pombe za kienyeji, ambapo mara nyingi wananchi wakitoka kwenye shughuli zao za kilimo huketi pamoja na kupata kiburudisho.

Ngoma za asili za wakazi wa Manda ni mganda, kihoda na ligambusi.

Hata hivyo, ngoma yao kuu ya kiutamdauni ni mganda ambayo huchezwa zaidi na kabila la Wamanda na Wakisi kutoka pembezoni kabisa mwa Ziwa Nyasa.

Mganda ni ngoma inayochezwa na vijana wa kiume watanashati, maridadi na wanaovalia kaptula nyeupe, soksi ndefu nyeupe, raba nyeupe, mashati meupe ya mikono mirefu na kofia nyeupe aina ya bareti na huwa wanashika mikia ya ng’ombe mkono mmoja na mwingine wameshika kikonyo cha kibuyu kilichofungwa karatasi ya nailoni.

Ngoma hii huchezwa kwa mtindo wa aina yake, inafurahisha na kushawishi kutazama, wachezaji hujipanga mstari ili kutoa nafasi ya kucheza na kabadili staili kadiri inavyoruhusu.

Pia kuna ngoma aina ya lindeku ambayo yenyewe wanaume na wanawake hupenda kucheza katika sherehe mbalimbali hasa katika nyakati za msimu baada ya mavuno au shughuli za kisiasa.

Shughuli za uzalishaji za Wamanda

Wamanda wa Wilaya ya Ludewa wamejaaliwa kuwa na utajiri mkubwa wa makaa ya mawe na chuma, hata hivyo wananchi wake bado wana hali mbaya ya kiuchumi.

Shughuli kubwa za uzalishaji zinazofanywa na watu wa jamii ya Wamanda ni kilimo na uvuvi, lakini kuna rasilimali zingine kama vile maliasili yakiwemo madini ya aina mbalimbali ambayo bado hayajaanza kuleta matunda kwa wananchi husika.

Chakula kikuu cha Wamanda ni ugali wa muhogo na samaki na shughuli kuu ya uchumi ya watu wa jamii ya Wamanda ni pamoja na uvuvi wa samaki na ukulima wa mazao madogomadogo.

Wamanda kwa kiasi kikubwa wanazungumza lugha ya Kimanda yenye mchanganyiko wa Kingoni na Kinyasa. Lakini pia lugha hiyo ina maneno mengi ya Kiingereza.

Wamanda walio wengi ni Wakristo wa madhehebu ya Anglikana na Katoliki japo kuna idadi ndogo ya Wamanda wanaoendelea kufuata dini za kiasili, na wengi wao bado wana mazoea ya kuendelea kuienzi mizimu na mahoka.

Wakati wa mkoloni na mara baada ya uhuru Wamanda wengi walifanikiwa kusoma na kuwa na elimu nzuri. Hata hivyo, idadi yao katika nafasi za juu za uongozi ni chache sana.

Mazingira ya Wamanda Mji mdogo wa Manda upo kwenye mwambao wa Ziwa Nyasa karibu na mdomo wa Mto Ruhuhu mpaka Lupingu.

Eneo lote la Manda lina vivutio vingi sana, ikiwemo ufukwe maridhawa wa Ziwa Nyasa, aina mbalimbali za samaki kama mbasa, ngumbu, mbelele, mawoma na Milima ya Livingstone.

Ukiwa juu ya Milima ya Livingstone utaliona Ziwa Nyasa vizuri sana na nchi ya Malawi ambayo zamani ilikuwa inaitwa Nyasaland.

Mto Ruhuhu ndiyo mto mkubwa unaoingiza maji katika Ziwa Nyasa, si kwa upande wa Tanzania tu. Hakuna mto mwingine mkubwa unaoingiza maji Ziwa Nyasa zaidi ya Mto Ruhuhu.

Upande mmoja wa Mto

Ruhuhu kuna kijiji cha Kipingo na upande mwingine kuna kijiji cha Lituhi. Mila moja kubwa sana ya Wamanda ni kuzuru kila mwaka makaburi.

Hii ndiyo sababu kubwa sana ya Wamanda kupenda kurudi kwao wakati wa likizo zao.

Manda pia kuna Kanisa kubwa la Anglikana la Mtakatifu Thomaso na bandari ya kale ya MandaWiedhafen.

Hapo kuna mbuyu mkubwa ambao una kibao cha heshima ya Mdachi aliyejitolea kupigana vita upande wa Wajerumani, lakini alifia eneo la Ruanda, Wilaya ya Mbinga.

Pia kuna kanisa kubwa la Katoliki pale Lituhi, kanisa ambalo lilijengwa mwaka 1942. Makanisa mengine ya Katoliki yapo Ngelenge, Nsungu na Igalu. Kwa ujumla vijiji vyote vya Manda vina makanisa ya Anglikana na Katoliki.

Elimu Wamanda wamebahatika kupata elimu kutokana na misingi ya misheni za Anglikana na Katoliki, maana shule zote zilikuwa za misheni. Ndiyo maana Wamanda wengi ni Wakristo wa Anglikana na Katoliki.

Kati ya Wamanda wametokea maprofesa, madaktari na wanasiasa maarufu kama hayati Horace Kolimba, mwanasheria kitaaluma (kati ya wanafunzi wa kwanza walioanza kusoma Chuo Kikuu cha Dar es Salaam pale Mnazi Mmoja - leo Chuo wa Watu

Wazima (Institute of Adult Education), aliyekuwa Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambaye aliweka misingi imara ya chama.

Wengine ni Profesa Crispini Haule ambaye alikuwa Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Profesa Raphael Mwalyosi aliyekuwa mbunge wa Ludewa kuanzia mwaka 2005 hadi 2010, na Dk Aleck Cheponda, mwasisi wa chama cha siasa cha Tanzania People’s Party (TPP).

Dk Cheponda alikuwa mwanasiasa na msomi wa sayansi ya siasa na aliwahi kuwa Mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Idara wa Sayansi na Utawala kati ya mwaka 1980 na 1991.

Wapo pia Dk Christopher Mlosy Ndomba, mchumi ambaye anafanya kazi katika Shirika la Utafiti wa Sayansi na Viwanda la Afrika Kusini (CSIR), na kabla ya kujiunga na CSIR alikuwa mtaalamu katika Shiririka la Kazi la Umoja wa Mataifa (ILO) na wengineo.

Kwa sasa kiwango cha elimu kwa Wamanda kiko chini kwa sababu mbalimbali ikiwemo upungufu wa walimu katika shule za kata na hali ngumu ya uchumi inayosababisha wanafunzi wengi washindwe kumaliza japo kidato cha nne.

Makala haya yametokana na vyanzo mbalimbali vya habari. 0685 666964 au [email protected]

Join our Newsletter