Uko hapa: NyumbaniHabari2021 11 25Article 574030

Habari za Mikoani of Thursday, 25 November 2021

Chanzo: mwananchidigital

Wanafunzi 34,000 waacha masomo Mara

wanafunzi 34,000 waacha masomo Mara wanafunzi 34,000 waacha masomo Mara

Zaidi ya watoto 34,000 waliondikishwa kuanza elimu ya Msingi kuanzia mwaka 2017 hadi mwaka huu mkoani Mara hawapo shuleni na hawajulikani walipo.

Takwimu hizo zimetolewa leo Novemba 25, 2021 mjini hapo na Mkuu wa Mkoa huo, Ally Hapi wakati akifungua kikao cha kamati ya ushauri ya mkoa (RCC) ambapo amesema kuwa hali hiyo inatokana na tatizo la utoro sugu ndani ya mkoa.

Amefafanua kuwa katika kipindi hicho jumla ya watoto 316,000 waliandikishwa kuanza elimu ya msingi na kwamba kati yao asilimia 10.8 hawajulikani walipo jambo ambalo amesema kuwa ni hatari kwa ustawi wa jamii.

"Tulifanya tathmini katika shule zetu za msingi na kubaini kuwa watoto zaidi ya 34,000 hawajulikani walipo kwani hawajahitimu, shuleni hawapo huku taarifa zikidai wengine wapo kwenye ajira huko migodini, wengine wanavua samaki na wengine wakichunga ng'ombe," amesema Hapi.

Kufuatia hali hiyo amewaagiza wakuu wa wilaya pamoja na kamati zao za ulinzi na usalama kuanza kufuatilia walipo watoto hao ili wawarejeshe shuleni.

"Wazazi waulizwe watoto wako wapi na sheria ichukue mkondo wake hatuwezi kukaa kimya hatujui watoto wako wapi.

“Inawezekana wamechukuliwa na kupelekwa kwenye shughuli haramu labda wako porini wanafundishwa mambo maovu mwisho wa siku tunakuwa na jamii mbovu," amesema Hapi

Amesema kuwa endapo hali hiyo haitadhibitiwa mapema upo uwezekano wa kujenga jamii yenye watu wasiokuwa na maadili wakiwepo majambazi, matapeli, vibaka na watu wenye tabia zisizofaa katika jamii na nchi kwa ujumla.

Hapi amesema kuwa tatizo la utoro pia ni miongoni mwa sababu zinazosababisha Mkoa wa Mara kufanya vibaya katika mitihani ya kitaifa hasa kwa shule za msingi na kidato cha pili na cha nne na kwamba ili kuondokana na hali hiyo tayari mkoa umeanza kutafuta suluhisho la tatizo hilo ikiwa ni pamoja na kutokomeza visababishi.