Uko hapa: NyumbaniHabari2021 08 12Article 551227

Habari za Mikoani of Thursday, 12 August 2021

Chanzo: ippmedia.com

Wanafunzi 710 wafundishwa na walimu saba

Wanafunzi 710 wafundishwa na walimu saba Wanafunzi 710 wafundishwa na walimu saba

SHULE ya Msingi Kambarage iliyopo Kijiji cha Kakisheri, Musoma Vijijini mkoani Mara, ina jumla ya wanafunzi 710 na walimu saba tu, hali ambayo inasababisha ufundishaji na ujifunzaji kukabiliwa na changamoto.

Mwalimu mkuu wa shule hiyo Gerala Wanyaka, amesema kuwa walimu wanaohitajika ni 15 huku akiongeza kuwa madarasa yanayohjitajika ni 16, yaliyopo ni nane na pia matundu ya choo yanatakiwa 22, lakini yapo 15.

"Kuna mrundikano mkubwa wa wanafunzi kutokana na uhaba wa vyumba vya madarasa, lakini pia tunakabiliwa na uhaba wa nyumba za walimu, kwani zinahitajika 15, lakini zipo tatu tu," amesema Wanyaka.

Amefafanua kuwa wanafrunzi 112 wa darasa la sita wanatumia chumba kimoja cha darasa hali ambayo inasababisha ufundishaji na ujifunzaji kukabiliwa na changamoto hasa kwa upande wa usikivu.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Kakisheri, Maridadi Magafu amesema, wakazi wa kijiji hicho wameanza kuchimba msingi kwa ajili ya kujenga madarasa na mawili na ofisi moja ya walimu.

Amesema, wanasomba mawe, mchanga, maji na kokoto, huku wakichangia Sh. 4,200 kila mkazi wa kijiji hicho aliyefikisha umri wa miaka 18, kwa lengo la kuharakisha kazi ya kuongeza madarasa.

"Lakini pia kuna michango mbalimbali ambayo imetolewa na mbunge wetu Profesa Sospeter Muhongo ambaye ametoa madawati 100, mifuko 60 ya saruji mabati 54 na vitabu zaidi ya 1,000," amesema Magafu.

Ameongeza kuwa mdau mmoja wa elimu aliyemtaja kwa jina la Mauza Nyakirang'anyi, ametoa mbao za kupaua chumba kimoja cha darasa ambao ametoa wito kwa wadau wengine zaidi kusaidia ujenzi huo.

Mwenyekiti huyo amesema, shule hiyo ilianzishwa mwaka 2001, ikiwa ni jitihada za serikali za kusogeza huduma ya elimu karibu ili kuwapunguzia watoto kutembea umbali mrefu.