Uko hapa: NyumbaniHabari2021 05 29Article 540490

xxxxxxxxxxx of Saturday, 29 May 2021

Chanzo: ippmedia.com

Wanafunzi 750 wasaidiwa taulo za kike

Msaada huo ulitolewa Taasisi ya Flaviana Matata Foundation, jana ikiwa ni maadhimisho ya kilele cha Siku ya Hedhi Salama Duniani, ambayo huadhimishwa Mei 28 ya kila mwaka.

Akizungumzia mgawanyo wa taulo hizo, mkurugenzi wa taasisi hiyo Flaviana Matata alisema, 480 kati ya hizo zimepelekwa Dodoma na nyingine 270, kwa wanafunzi wa Sekondari ya Kiembe Samaki Islamic Zanzibar.

"Kila sehemu tuna mwakilishi wetu, hivyo kule Dodoma taulo zitakabidhiwa kwa maofisa wa elimu ili waone ni shule gani watakwenda kuzigawa, kule  Zanzibar zinapelekwa Kiembe Samaki Islamic Sekondari," alisema Flaviana.

Mkurugenzi huyo alisema, Siku ya Hedhi Duniani huadhimishwa kwa kuwakutanisha wadau mbalimbali wadau kwa lengo la kuongeza uelewa kuhusu masuala ya hedhi na kuhamasisha upatikanaji maji safi na taulo wasichana/wanawake.

Alifafanua kuwa, maadhimisho hayo yanatoa elimu ya kuwa na hedhi salama ambayo inahusisha mtoto wa kike/mwanamke kupata mahitaji yake yote muhimu atapokuwa kwenye hedhi.

"Hatua hiyo inatakiwa kwenda sambamba na upatikanaji  wa  taulo za kike au pedi, hivyo sisi kama taasisi tumekuwa tukijitahidi kutoa msaada wa vifaa hivyo katika kila maadhimisho," alisema.

Alisema, walengwa zaidi ni wale ambao wapo katika mazingira magumu ili wanapoingia katika siku zao, waweze kujisitiri na kuendelea na shuguli zao na kuhudhuria masomo kama kawaida.

"Suala la hedhi halipaswi kuwa kero kwa mtoto wa kike, lakini imekuwa tofauti kwa watoto wengi wa kike ambao wamekuwa wakipata wasiwasi na kukosa raha wanapokaribia mzunguko wao," alisema.

Alisema, mazingira hayo pia husababisha mtoto wa kike kutojihusisha katika shughuli mbalimbali za jamii kutokana na kukosekana kwa nyenzo za kumsaidia anapokuwa kwenye hedhi.

"Wataalamu wa afya wanasema, mtoto wa kike akipata hedhi salama, anaweza kuondokana na matatizo ya kiafya ikiwamo miwasho, fangasi na magonjwa mengine, hivyo hedhi yenye amani na furaha ni muhimu," alisema.

Aidha, Flaviana alishauri kuwa, kama ikiwezekana, wavulana nao washirikishwe katika kupata elimu ya masuala ya hedhi kama washiriki wenza na pia kiini cha mabadiliko.

Join our Newsletter