Uko hapa: NyumbaniHabari2021 11 18Article 572530

Habari za Mikoani of Thursday, 18 November 2021

Chanzo: mwananchidigital

Wananchi wachoma nyumba ya mganga wa zahanati Nkasi

Wananchi wachoma nyumba ya mganga wa zahanati Nkasi Wananchi wachoma nyumba ya mganga wa zahanati Nkasi

Wananchi wa kijiji cha Nkundi kata ya kipande wilayani Nkasi mkoani Rukwa wamechoma nyumba ya mganga wa zahanati ya Nkundi, Marko Lazaro kwa madai kuwa ameshindwa kutoa huduma hali iliyosababisha mama mjamzito kufariki dunia.

Diwani wa kata ya Kipande, Joseph Mwenda amesema kuwa tukio hilo limetokea Jumanne Novemba 16, 2021 ambapo wananchi kwa ujumla wao walikwenda kuichoma nyumba ya mganga huyo, ambayo ni mali ya Serikali kwa madai kuwa mganga huyo kutokuwepo kwa muda mrefu kituoni hapo hali inayofanya wagonjwa kukosa matibabu pindi wanapofika kituoni hapo.

Amesema kutokana na kitendo cha mganga huyo, kutokuwepo kazini kwake kwa muda mrefu, kuna watu wengi wamepata changamoto ya kukosa huduma kwa wakati ikiwamo mama mjamzito hali iliyosababisha kupoteza maisha.

Diwani huyo amedai kuwa wao walishapeleka malalamiko yao muda mrefu kwa mwajiri wake wakiamini kuwa hatua zitachukuliwa kwa haraka, lakini bado vitendo vya mganga huyo kutokuwepo kazini viliendelea.

Mganga Mkuu wa Wilaya Nkasi, Benjamini Chota amesema kuwa baada ya tukio hilo kutokea yeye na timu yake ya wataalamu walikwenda moja kwa moja kijijini hapo, ambapo wao walifanya uchunguzi na kuwahoji baadhi ya watu juu ya tukio hilo hivyo kuamua kuondoka na mganga huyo wa zahanati na kumpeleka makao makuu ya wilaya.

Mganga huyo Marko Lazaro ambaye nyuma aliyokuwa akiishi imechomwa amesema kuwa baada ya nyumba yake kuchomwa baadhi ya raia wema walikwenda kumuokoa ikiwa ni pamoja na kufanikiwa kuuzima moto kabla haujafanya madhara makubwa.

Juu ya madai ya yeye kutokuwepo kazini siku nyingi, amedai kuwa ni kweli kwani muda mrefu alikua akimuuguza mke wake mjini Sumbawanga.