Uko hapa: NyumbaniHabari2021 06 06Article 541240

xxxxxxxxxxx of Sunday, 6 June 2021

Chanzo: www.habarileo.co.tz

Wananchi wahadharishwa madalali ‘Takukuru’

TAASISI ya Kuzuia na Kupambana Rushwa (TAKUKURU), imewatahadharisha wananchi dhidi ya madalali ambao ni matapeli wanaojifanya kuwa wanatoa huduma mbalimbali za taasisi hiyo.

Taarifa iliyotolewa na Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano, Doreen Kapwani ilisema matapeli hao wamekuwa wakiwapigia wananchi pamoja na watumishi mbalimbali wakisema wanahusika katika upangaji wa ratiba ya kuonana na Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru, Kamishna wa Polisi, Salum Hamduni.

Alisema Takukuru inawapongeza baadhi ya wananchi walioweza kuwatambua na kutoa taarifa katika taasisi hiyo mara moja. Alisema Takukuru ina utaratibu wake wa mawasiliano au kuwaita watuhumiwa au mashahidi ofisini.

Alisema utaratibu huo unajumuisha kutuma hati ya wito (samansi) kufika katika ofisi za Takukuru pamoja na kuujulisha uongozi kwa maandishi ikiwa mhusika ni mwajiriwa kama ilivyo utaratibu wa mawasiliano serikalini.

Taarifa hiyo iliwataka wananchi kujiridhisha na mtu yeyote atakayewapigia simu kwa kuwasiliana na Takukuru kwa kupiga simu bure kupitia namba ya simu ya dharura ambayo ni 113 inayopatikana kwa saa 24 au kupitia barua pepe [email protected]

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, wananchi wanaweza kueleza wasiwasi wao juu ya wito walioupata bila kusahau kutaja namba ya simu iliyowasiliana naye kwa kupiga namba zifuatazo; 0738150100 au 0738150046.

Taasisi hiyo imetoa onyo kwa matapeli wote wanaojihusisha na udalali huo kuwa namba zao zote zipo katika mikono yake na taratibu mbalimbali zinakamilishwa ili hatua stahiki zichukuliwe.

Join our Newsletter