Uko hapa: NyumbaniHabari2021 08 12Article 551260

Habari za Afya of Thursday, 12 August 2021

Chanzo: www.habarileo.co.tz

Wanandoa jitokezeni kupata chanjo

Wanandoa jitokezeni kupata chanjo Wanandoa jitokezeni kupata chanjo

WANANDOA wamehimizwa kujitokeza kwa wingi kwa ajili ya kupata chanjo ya Corona ili waweze kujikinga na virusi vya mlipuko wa ugonjwa huo.

Hayo yametolewa na Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Mwanaidi Ali Khamis.

Pia amewataka wazee kuanzia umri wa miaka 50 na watu wenye magonjwa sugu kujitokeza kwa wingi kupata chanjo ya Corona kwa kuwa ni salama na imethibitishwa na wataalamu wa afya.

Mwanaidi ametoa kauli hiyo wilayani Songea Mkoani Ruvuma wakati wa ziara yake mkoani humo kukagua huduma za matibabu kwa Wazee katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa.

Amewataka Maafisa Ustawi wa Jamii na Maafisa Maendeleo ya Jamii kuendelea kutoa elimu na kuwahamasisha Wazee kuanzia umri wa miaka 50 kujitokeza kwa hiari yao kupata Chanjo ya Corona.

"Awamu hii ya utoaji wa Chanjo ya UVIKO19 tumewapa kipaumbele wazee kuanzia miaka 50 kupata Chanjo ya UVIKO19 ili kusaidia kupata kinga itakayowalinda na maambukizi ya Virusi vya Corona" alisema Mwanaidi

Aidha, Mwanaidi amewahimiza wanandoa walio na umri wa miaka 50 na kuendelea kuhimizana kupata Chanjo ya UVIKO19 ili waweza kujikinga na virusi vya Corona.

Kwa upande wake Afisa Maendeleo ya Jamii Mkoa wa Ruvuma Mariam Juma, amesema kuwa wataendelea kuhamasisha jamii hasa kundi la wazee na watu wenye magonjwa sugu kujitokeza kwa hiari yao kupata Chanjo ya UVIKO19.