Uko hapa: NyumbaniHabari2022 01 11Article 584821

Habari Kuu of Tuesday, 11 January 2022

Chanzo: www.tanzaniaweb.com

Wanansiaa acheni siasa za chuki- Dk Mwinyi

Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Dk. Hussein Ali  Mwinyi Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Dk. Hussein Ali Mwinyi

Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi amewataka wanasiasa kuhakikisha kauli zao zinalenga kuwaunganisha wananchi na si kuwagawa.

Aidha, amewataka kufanyakazi kwa kuweka mbele maslahi ya taifa na uzalendo.

Dk Mwinyi alitoa rai hiyo wakati akizindua kikosi kazi ambacho kinatokana na mkutano wa vyama vya siasa wa Baraza la Demokrasia uliofanyika Dodoma mwaka jana na kupewa majukumu ya kupitia mambo ya msingi yanayotokana na maazimio ya wadau wa mkutano huo.

Aliwataka wajumbe wa kikosi hicho kufanyakazi kwa kuweka mbele maslahi mapana ya taifa na kuacha kuiga siasa za mataifa ya nje ambazo kwa upande wa Tanzania haziwezi kufanya kazi vizuri.

Alikitaka kikosi kazi hicho kuweka mbele maslahi ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ambao ni matokeo ya Mapinduzi ya Januari 12 mwaka 1964 yaliyowakomboa Wazanzibari kuwa huru katika nchi yao.

‘’Nimefurahishwa na kikosi kazi hiki chenye mchanganyiko wa wajumbe wenye uwezo na uzoefu katika demokrasia ya siasa za vyama vingi, kazi yenu ni kuchambua na kupitia mambo ya msingi yenye mustakabali mwema kwa taifa letu,’’ alisema.

Dk Mwinyi aliahidi kwamba serikali zote mbili, Muungano na Zanzibar zitatoa ushirikiano wa dhati kwa kikosi kazi hicho ili kuhakikisha changamoto zote zinapatiwa ufumbuzi na kuyafikia malengo.

Alisema tangu Tanzania kuingia katika mfumo wa vyama vingi takribani miaka 29 sasa, mafanikio makubwa yamefikiwa ikiwamo kuwapo kwa maridhiano ya kisiasa yenye lengo la kuimarisha amani na utulivu.

Awali, Mwenyekiti wa kikosi kazi hicho, Profesa Rwekaza Mukandala alisema chombo hicho ni matokeo ya mkutano uliowakutanisha wadau wa vyama vya siasa na demokrasia mjini Dodoma mwaka jana ili kuzipatia ufumbuzi changamoto zote zinazokwaza vyama vya siasa katika utekelezaji wa majukumu yao.

Miongoni mwa mambo ambayo yalijadiliwa na wajumbe wa mkutano wa vyama vya siasa na kutaka kufanyiwa kazi ni Katiba mpya, Tume Huru ya Uchaguzi, vyama vya siasa kuzuiwa kufanya mikutano na Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora.

‘’Hiki ni kikosi kazi ambacho ni matokeo ya mkutano ambao wewe Rais wa Zanzibar ulikuja Dodoma na kutufungia baada ya Rais wa Jamhuri ya Muungano, Samia Suluhu Hassan kuufungua,’’ alisema.

Naye Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Othman Masoud Othman alisema uzinduzi wa kikosi kazi hicho ni moja ya safari mpya ya kuelekea katika utekelezaji wa demokrasia yenye tija kwa maslahi ya wananchi wote.

Aliwataka wajumbe wa kikosi kazi kuzingatia uzalendo na ushirikishaji watu wengi ili kufikia malengo yaliyokusudiwa.