Uko hapa: NyumbaniHabari2021 09 24Article 559396

Habari za Mikoani of Friday, 24 September 2021

Chanzo: www.habarileo.co.tz

Wanaochanja Covid 19 waongezeka Kigoma 

Wanaochanja Covid 19  waongezeka Kigoma  Wanaochanja Covid 19 waongezeka Kigoma 

SERIKALI mkoani Kigoma imesema kumekuwa na ongezeko kubwa la watu wanaojitokeza kupata chanjo ya Ugonjwa wa Covid-19 tangu kuanza kwa mpango wa uchanjaji shirikishi na harakishi unaoendeshwa na Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto.

Mganga Mkuu wa Mkoa Kigoma, Dk Simon Chacha, akifungua mafunzo ya siku tano kwa wahudumu wa afya ngazi ya jamii kuhusu kuzuia maambukizi ya Covid-19 na uhamasishaji ya chanjo kwa jamii yanayoendeshwa na taasisi ya afya ya Medical Team International, alisema elimu na uhamasishaji huo umechangia kuongezeka kwa watu wanaojitokeza kupata chanjo.

Dk Chacha alisema mkoa ulipokea dozi 40,000 ambapo dozi 35,000 zimeshatumika kwa watu kuchanja na kwamba mipango imewekwa kuhakikisha uchanjaji unarahisishwa kwa kuweka vituo vya muda katika maeneo mbalimbali yenye mikusanyiko ya watu.

Akitoa maelezo kuhusu mafunzo hayo, Mratibu kutoka Shirika la Medical Team International, Magdalena Mwaikambo, alisema jumla ya wahudumu wa afya 920 kutoka wilaya za Kasulu na Kibondo watapatiwa mafunzo ili kutoa chanjo yenye viwango vinavyokubalika lakini kutoa hamasa na uelewa kwa jamii kuhusu utoaji wa chanjo hiyo.

Mmoja wa washiriki wa mafunzo hayo, Masika Malulu, mhudumu wa afya ngazi ya jamii, alisema kuwa mafunzo hayo yatakuwa chachu kwao kuwa na taarifa sahihi ambazo zinapaswa kufikishwa kwa jamii ili kuondoa dhana potofu kuhusu chanjo.