Uko hapa: NyumbaniHabari2021 06 23Article 543823

Diasporian News of Wednesday, 23 June 2021

Chanzo: www.habarileo.co.tz

Wanaoingia Zanzibar shurti cheti chanjo ya Covid-19

Wanaoingia Zanzibar shurti cheti chanjo ya Covid-19 Wanaoingia Zanzibar shurti cheti chanjo ya Covid-19

SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) imeanza kuchukua tahadhari ya ugonjwa wa Covid-19 awamu ya tatu na kutangaza wageni wote watakaoingia nchini kuhakikisha wanakuwa na vyeti vya chanjo vya ugonjwa huo.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Afya, Ustawi wa Jamii, Jinsia na Watoto, Nassor Ahmed Mazrui wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu tahadhari ya ugonjwa huo kutokana na taarifa za kuingia kwa wimbi la tatu.

Mazrui alisema zipo baadhi ya nchi jirani zenye mahusiano makubwa na Tanzania ikiwemo Uganda, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo(DRC) pamoja na Rwanda tayari wimbi la tatu la ugonjwa wa Covid-19 limeingia na serikali za nchi hizo zimetangaza karantini kudhibiti athari zaidi.

Aidha alisema kwa upande wa wizara tayari imejipanga kukabiliana na janga hilo kwa kutoa elimu kwa wananchi kuhusu dalili za ugonjwa huo huku vituo vyote vya afya vikiwekwa tahadhari za ziada.

‘’Wizara ya Afya inatoa tahadhari kwa wananchi kuhusu ugonjwa wa Covid-19 awamu ya tatu ambapo baadhi ya nchi za Ulaya na Asia umeanza kusababisha maafa makubwa na nchi jirani ya Tanzania...kuanzia sasa wageni wote watakaoingia nchini watalazimika kuonesha cheti cha chanjo kwa ugonjwa huo,’’alisema.

Aidha aliitaja mikakati mingine inayotarajiwa kuchukuliwa kukabiliana na janga hilo ikiwemo wananchi kuvaa barakoa pamoja na kuepuka mikusanyiko ya watu wengi isiyokuwa na sababu za lazima.

Kuhusu suala la chanjo ya corona kwa wananchi wa Zanzibar, alisema suala hilo linasubiri tangazo rasmi la Rais Samia Suluhu Hassan ambaye ndiye mwenye uamuzi wa mwisho.

Awali Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Mnazi mmoja Dk Abdallah Suleiman alisema wamejipanga kuhakikisha wafanyakazi wote kuanzia vituo vya afya hadi hospitali kuu wapo tayari kutoa huduma za dharura kwa wagonjwa watakaojitokeza wa Covid-19.

Alisema hadi sasa hakuna mgonjwa aliyetambuliwa kuambukizwa na ugonjwa huo huku akisisitiza hakuna taarifa za kuficha matukio ya ugonjwa huo.