Uko hapa: NyumbaniHabari2021 06 26Article 544270

Dini of Saturday, 26 June 2021

Chanzo: www.habarileo.co.tz

Wanawake Wakatoliki wampongeza Samia

Wanawake Wakatoliki wampongeza Samia Wanawake Wakatoliki wampongeza Samia

WANAWAKE Wakatoliki Tanzania (Wawata) wamempongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kupokea uongozi kwa amani na utulivu mkubwa na wamemhakikishia kuwa hawatamzingua, bali wako pamoja naye katika ustawi wa maendeleo na mafao ya Watanzania wote.

Akizungumza katika mkutano wa Baraza la Maaskofu Tanzania (TEC) ambao Rais Samia alizungumza na maaskofu jana, Kurasini, Dar es Salaam, Mwenyekiti wa Wawata, Everlyne Ntenga, amesema umoja huo unamshukuru Mungu kwa kumpata rais mwanamke aliye jasiri na wanamuombea afya njema.

“Tunamshukuru Mungu kutufikisha hapa taifa tukiwa na amani na utulivu, jambo ambalo tunaamini hata dunia inashangaa. Tunapenda kukupongeza kwa moyo wa utumishi, moyo wa uvumilivu, unyenyekevu na ujasiri kupokea kijiti cha Serikali ya Awamu ya Sita katika kipindi kigumu cha majonzi. “Na sasa kazi inandelea. Sisi akina mama tunakuombea kwa Mungu daima, wewe pamoja na viongozi wasaidizi wako wote kwa maana tuna wajibu wa kufanya hivyo. Mungu awajalie ari na moyo wa kishujaa kuendeleza na kutafuta mafao ya wananchi na kuendelea kulitumikia taifa,” alisema Luena.

Alimuahidi kuwa Wawata wapo pamoja naye, hawatamuangusha.

“Tutaendelea kudemka pamoja na wewe katika ustawi wa maendeleo na mafao ya Watanzania wote. Mungu akulinde, akubariki katika uongozi wako na daima umoja na mshikamano wa Watanzania wote ukapewe vipaumbele.”

Aliushukuru uongozi wa TEC kwa kuwashirikisha walei katika shughuli za ujenzi wa kanisa.

Alitumia fursa hiyo kumuomba Rais Samia awe mgeni rasmi katika maadhimisho ya miaka 50 ya Wawata yatakayofanyika Septemba mwakani kuona shughuli zao kwa kanisa na taifa. Wawata ilianzishwa mwaka 1972.

Akijibu ombi hilo Rais Samia katika hotuba yake alisema, “Niwashukuru wamama wa kanisa kwa miaka 50 ya walei (Wawata) nawapongeza sana. Niseme nimepokea mwaliko wenu, mkiniletea tarehe tukikutana tutazungumza yetu ya kike. Asanteni kwa zawadi.”

Akitoa historia ya TEC, nchini Tanzania, Askofu Msaidizi wa Jimbo la Bukoba, Method Kilaini alisema baraza hilo ndio msingi wa kanisa na lilianza na ujio wa Kanisa Katoliki nchini kupitia Wamisionari wa kwanza mwaka 1860 waliofikia Zanzibar baadaye mwaka 1868 walifika Bagamoyo kupitia Shirika la Roho Mtakatifu na kisha wakasambaa Kilimanjaro mwaka 1890, Arusha na Tanga na kwingineko.

Kilaini alisema kundi jingine lilifika mwaka 1878 Wamisionari wa Afrika, wakaenda maeneo ya Tabora na Magharibi mwa Tanzania. 1887 Wabenedictine walifika Dar es Salaam na kuelekea Songea na Mtwara.

Mambo yao matatu muhimu ni kueneza dini, kuwatibu wagonjwa na kuwafundisha watu wajue kusoma kuandika na kuhesabu.