Uko hapa: NyumbaniHabari2021 08 16Article 551692

Habari za Afya of Monday, 16 August 2021

Chanzo: www.mwananchi.co.tz

Wanawake waongoza kwa "UDOKOZI"

Sababu za tabia ya udokozi Sababu za tabia ya udokozi

Umewahi kufikiria kama kuna ugonjwa wa udokozi? Wanasaikolojia wanasema wale watu katika jamii wenye tabia ya udokozi, wana ugonjwa wa kisaikolojia ujulikanao kitaalamu kama ‘kleptomania’.

Mwananchi ilifanya utafiti mdogo na kubaini watu wengi wanaonasibishwa na ugonjwa huo ni wanawake wakiwamo wasichana.

Miongoni mwa watu waliozungumzia tatizo hilo ni Rehema Mapunda (50), mkazi wa Magomeni Mapipa, Dar es Salaam ambaye anasema ni miongoni mwa walioathiriwa na ugonjwa huo.

“Nilipokuwa mtoto, nilipenda kudokoa mboga, hata kama tumetoka kula na nimeshiba, lakini nikiingia jikoni tu nikiona chungu, lazima nidokoe na kubugia,” anasimulia Rehema.

Anasema hata alipokuwa msichana aliendelea na tabia hiyo, kwani alikuwa akiwadokolea wenzake vitu mbalimbali yakiwamo mafuta ya kupaka, vitambaa vya mkono, wanja na lipstiki.

Jaqueline George anasema amekuwa akidokoa fedha za mumewe kila mara, hasa nyakati za usiku anapokuwa amelala.

“Kusema ukweli mimi sina shida, mume wangu ananipa kila kitu, lakini huwa najisikia tu kumchomolea hela zake kwenye pochi. Nategea usiku akirudi matembezi akiingia chumbani kulala, akiwa kalala fofofo naamka napekua suruali yake hela yoyote nitakayoikuta ni halali yangu,” anaeleza Jaqueline.

Naye mwanafunzi wa Shule ya Sekondari Jangwani ambaye hakutaka jina lake litajwe gazetini, anasema amekuwa bingwa wa kudokoa vifaa vya shule vya wenzake, zikiwamo soksi na sare za shule.

“Hahahahaaa kwa kweli mimi ugonjwa huu ninao haswa, yaani naweza nikawa na vifaa vyangu vyote vya shule, lakini nikimuona mwenzangu bwenini kanunuliwa shati jipya, soksi au sketi, huwa natamani kumuibia. Halafu nikiiba wakati mwingine hata kuvaa sivai naitazama tu,” anasema mwanafunzi huyo.

Hata hivyo, kwa mujibu wa jarida la saikolojia lijulikanalo kwa jina la International review of psychiatric (2020) katika ukurasa wa 451 hadi 454, ugonjwa huo huwapata watu wa jinsia zote, lakini wanaoathiriwa zaidi ni wanawake kwa kuwa wanapenda kuiba vitu vidogo ambavyo wanaweza kuvinunua.

Jarida hilo limeandika watu wenye ugonjwa huo hawaendi hospitalini kupata tiba kutokana na ukweli kwamba wengi huona aibu au hawajitambui kuwa wanaumwa.

Ugonjwa huo unaweza kuwa chanzo cha hali mbaya ya uchumi wa mgonjwa mwenyewe, familia yake, taasisi, jamii na Taifa.

Jarida hilo limeendelea kuandika kuwa ugonjwa huu pia unaweza kusababisha kuvunjika kwa ndoa, migogoro ya kifamilia na hata ya kijamii.

Mwananchi lilizungumza na Mwanasaikolojia, Charles Kalungu ili kufahamu undani wa ugonjwa wa kleptomania.

Kalungu anasema kleptomania ni tatizo la kisaikolojia linalomsukuma mtu kuwa na hamu ya kuiba vitu vidogovidogo ambavyo havina thamani na wakati mwingine vinaweza kuwa havina maana au umuhimu wowote.

“Kwa mfano unakuta mtu anaiba mchele, ili atafune tu au anaamka usiku kudokoa wali, anaiba vibanio vya nguo au anaiba karatasi nyingi halafu wala hana matumizi nazo au labda anaiba soksi, nguo za ndani, mkanda wa suruali na vitu vingine kama hivyo,” anasema Kalungu.

Anasema mara nyingi watu wanaofanya hivyo huwa wakirudia mara kwa mara kwa sababu ya msisimko anaokuwa anaupata baada ya kufanya kitendo hicho.

“Kwa sababu ubongo huzalisha kemikali ya Dopamine ambayo huifanya tabia hii kujirudiarudia, wakati huo pia ubongo huzalisha kemikali ya Serotonin ambayo humchochea mtu kufanya kitendo hicho na kutarajia kupata furaha,” anasema.

Mwanasaikolojia huyo anasema kleptomania huwapata watoto na watu wazima na endapo isipodhibitiwa mapema inaweza kumsababishia mtu kuwa mwizi sugu.

Akizungumzia sababu zinazofanya mtu kupata ugonjwa huu, Kalungu anasema mojawapo ni urithishwaji wa vinasaba kutoka kwa wazazi kwenda kwa mtoto.

“Hapa nazungumzia mtu kurithi tabia hii kutoka kwa ndugu wa familia au wazazi wanaomlea,” anasema.

Pia, mtaalamu huyo anasema mazingira yanaweza kuchangia mtu kufikwa na hali hiyo, kwa sababu ya kushawishiwa hata kama alikuwa hapendi kufanya hivyo, anajikuta anaiba tu.

Anasema aibu iliyopitiliza nayo inaweza ikamfanya mtu kukumbwa na ugonjwa huo, kwa sababu anashindwa kuomba anachokitaka akihofia ataonekana ni mtu wa aina gani, hivyo anaona njia pekee na rahisi ni kuiba au kudokoa. Pia anasema hali hiyo inachangiwa na kutoridhika na kile akipatacho.

Dalilia za ugonjwa

Kwa mujibu wa Kalungu, dalili za ugonjwa huo ni pamoja na mtu kujawa na huzuni, kuwa na tamaa ya vitu vidogo pamoja na kupenda kujitenga na watu.

Kuhusu matibabu ya ugonjwa huo, anasema ni vema muathirika akapelekwa kwa wanasaikolojia ambao wataangalia asili ya tatizo au chanzo chake.

“Mtu wa saikolojia atakaa na mgonjwa na kumuuliza maswali mbalimbali kwa lengo la kubaini nini anachokihitaji hasa kwenye maisha yake.

“Pia tunaangalia kwa kiasi gani ameathirika na hali hiyo, huwa inamkuta mara ngapi kwa siku au wiki, pia tunaangalia mazingira aliyopo kama ni rafiki kwake,” anasema.

Anasema kwa kufanya yote hayo, mwanasaikolojia atapata ufumbuzi wa jinsi gani atamtibu kwa kumfanya aanze kubadili maisha aliyoyazoea na kumfundisha tabia mpya. Naye Daktari wa afya ya akili, Philimina Scarion kutoka Mental Health Tanzania anasema Kleptomania Disorder hutokea kama haikuambatana au kusababishwa na tatizo lingine la akili, mfano kuwa kichaa au kupata msongo wa mawazo (sonona).

“Mtu huchukua vitu vidogovidogo ambavyo anaweza hata kuwa havifanyii kazi yoyote,” anasema.

Kuhusu matibabu, Dk Philimina anasema ugonjwa huo umeegemea kisaikolojia zaidi, hivyo mgonjwa hukutanishwa na wanasaikolojia kwa ajili ya matibabu kama itakuwa haikusababishwa na magonjwa au matatizo mengine ya akili.

“Kama itakuwa imesababishwa na matatizo mengine kama ukichaa au msongo wa mawazo, kwanza hupatiwa dawa za kuondoa matatizo hayo kisha utatuzi wa Kleptomania hufuata,” anasema.