Uko hapa: NyumbaniHabari2021 06 11Article 542188

xxxxxxxxxxx of Friday, 11 June 2021

Chanzo: www.habarileo.co.tz

Wanyakyusa na historia yao ya kupendeza

LEO katika mwendelezo wa makala za utamaduni, mila na desturi za makabila mbalimbali ya Tanzania, tunaangazia jamii ya Wanyakyusa.

Wanyakyusa ni miongoni mwa makabila makubwa yaishiyo nchini. Wanapatikana Mkoa wa Mbeya katika Wilaya za Rungwe, Kyela na Ileje ingawa wameenea nchini na nchi jirani. Hapo mwanzo wilaya zote tatu zilikuwa ndani ya wilaya moja ya Rungwe.

Wenyeji wa wilaya zote tatu wanaongea lugha moja ya Kinyakyusa, hii ina maana kwamba wana utamaduni, mila na desturi zinazofanana kwa sababu kiasilia ni wamoja.

Inasemwa kuwa jamii ya watu wanaoitwa leo Wanyakyusa waliitwa Wakonde/Wangonde (pia walijulikana kama Wasokile), ndiyo maana hadi leo Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) linatumia jina “Dayosisi ya Konde” kwa eneo lake katika Mkoa wa Mbeya.

Kuanzia karne ya 20 “Wanyakyusa” limekuwa jina la kabila hilo kwa jumla.

Wakati Wajerumani walipofika sehemu za kaskazini mwa Ziwa Nyasa mwisho wa karne ya 19 hawakuona tofauti ya kimsingi kati ya watu wa Malawi Kaskazini na wale wa sehemu za Rungwe na hivyo wakawaita wote “Wakonde” kutokana na jina lililokuwa kawaida ziwani.

Historia ya Wanyakyusa

Nadharia ya kwanza inabainisha kuwa Wanyakyusa ni neno lililojengwa kwa jina “Kyusa”, sifa ukeni. Pia neno hilo limesimamia umoja na wingi, Wanyakyusa.

Inasemwa Kyusa ni jina la mke mdogo wa mfalme (Malafyale) kati ya wake zake wengi. Na neno “wanya” lina maana ya watoto wa fulani.

Jina hilo la Wanyakyusa, kutokana na masimulizi ya mapokeo kutoka kwa wazee, yasemekana kuwa mfalme alipokaribia kufa alihitaji mrithi, na hivyo palitokea mzee kikongwe mmoja (kuhani) ambaye alipita kila nyumba ya wake wa Malafyale ili kumtia mafuta atakayerithi ufalme.

Inasemekana kuwa kuhani huyo alikuwa kama mzee mchafu asiyetamanika kabisa. Katika nyumba zingine hakupata makaribisho mazuri (hawakumkirimu) na wala hakuona mtoto mwenye hekima ya kutawala na kuongoza.

Mwisho mzee huyo alikwenda kwenye nyumba ya mke wa mwisho wa malafyale aliyeitwa kwa jina la Kyusa kwa upande wa baba yake. Alipofika, alikaribishwa kwa ukarimu na kwa moyo mnyoofu uliochangamka.

Kwanza alipatiwa maji ya kuoga, halafu aliandaliwa chakula kinono. Aliposhiba alimuuliza malafyale kama ana watoto wa kiume katika nyumba ile. Walikuwepo vijana wakubwa lakini hawakupata kibali mbele ya mgeni huyo. Baadaye akauliza kama hakuna kijana mwingine.

Alijibiwa kuwa yupo lakini hayupo karibu, ila yuko malishoni (ndukubo). Mzee mgeni alimwomba malafyale atume wajumbe wake wamfuate huko malishoni. Na alipofika palifanyika sikukuu ya kumtia mafuta na kumtawaza awe malafyale.

Katika harakati ya kumpata mtawala kutoka kwenye nyumba ndogo ya Kyusa ndipo jamii zote zilipoanza kuitwa kwa sifa ya malkia kwa jamii ya Kyusa (Mnyakyusa kama ni mmoja na Wanyakyusa kama ni wengi).

Kama nilivyoainisha mwanzo, kabla ya hapo, Wanyakyusa walijulikana kwa jina la Wasokile. Hii ni kutokana na lugha yao nzuri ya kuamkiana, ambapo walisalimiana “mwemusokile” au “musokile” (habari ya kuamka) na kujibiwa “tusokile” (tumeamka salama) au “nsokile” (nimeamka salama).

Kubadilika kwa lugha kumetokana na nadharia ya mabadiliko na mwingiliano wa koo mbalimbali.

Historia inasema kwamba Wasokile ama Wanyakyusa wametokana na jamii ndogo ndogo nyingi. Lakini jamii kubwa ni tatu za Wanyakyusa Wabungu, Wanyakyusa Wanselya na Wanyakyusa Wangonde.

Wanyakyusa Wabungu wana majilio yao, na inaaminika kuwa ni watu waliotoka eneo la magharibi na maingilio yao ni Usangu ambapo walipitia Milima ya Ukinga-Umbwila na kuingia eneo la Rungwe.

Katika masimulizi yao wanasema kwamba waliwakuta wenyeji wa eneo hilo wanakula matunda na mizizi, wanyama na ndege. Kwa kuwa Wanyakyusa Wabungu walikuwa watu wenye nguvu na hodari wa kuwinda, kulima na kufuga ng’ombe, hivyo wenyeji waliwategemea sana kwa chakula na kwa usalama wao.

Wanyakyusa Wanselya walitokea eneo la mashariki kupitia Iringa na Mahenge na kuwakuta Wanyakyusa Wabungu wanaishi Rungwe kwa amani kabisa.

Wanyakyusa Wanselya wakiongozwa na Mwakapalila walipofika mwambao mwa Milima Rungwe-Kabale walidhani Wanyakyusa Wabungu wangewapiga kwa vile walivyokuwa wamesifika sana kwa amani na maendeleo.

Haikuwa hivyo na badala yake walishirikiana katika masuala ya kijamii kama vile ndoa, vifo na mambo mengine.

Wanyakyusa jamii ya Wanyangomole (Wangonde) inasemekana walitokea Malawi, yumkini walitoka Afrika Kusini kwa Wazulu na majilio yao yalitokana na vita na njaa kwa sababu ya ukame wa muda mrefu ambao ulisababisha vifo kwa watu wengi na mifugo pia. Hivyo walivuka Ziwa Nyasa kupitia Mto Songwe.

Masimulizi toka kwa wakazi wa eneo la Busokela, Rungwe Mashariki wanaungana na nadharia hii wakiamini kuwa asili yao ni Morogoro, ambapo walikimbia vita na hali mbaya ya hewa.

Wanasema kuwa mwindaji wa kabila la Kiluguru alifika katika eneo la Kabale lililopo Suma Rungwe na kukutana na Mzulu kutoka Afrika Kusini ambaye naye alikuwa mwindaji aliyekuwa na binti yake.

Kati ya wawindaji hao wawili, Mzulu alikuwa hafanikiwi kwenye mawindo yake wakati yule Mluguru alikuwa anafanikiwa kila mara. Mwisho alitokea kuwa mfadhili wa Mzulu na matokeo yake, Mzulu huyo alimpa binti yake kuwa mkewe.

Mluguru huyo akamwoa binti wa Kizulu na maisha yakaendelea huku nyumbani kwa mwindaji wa Kiluguru na mkewe kukiwa hakukosekani nyama kama kitoweo.

Kwa sababu ili kuihifadhi nyama ilibidi kwanza ibanikwe, basi kitendo hicho kilisababisha harufu nzuri ya kitoweo kile kusambaa eneo kubwa na kufika hadi ukweni kwake nyumbani kwa Mzulu. Mzulu alisema, “pale panatoa kyusi kila siku”, kwa maana ya moshi kwa lafudhi ya lugha ya Kizulu.

Kutokana na mazoea ya kutamka neno “kyusi” taratibu likageuka na kuwa Kyusa, na hivyo ikatokea kumwita Mluguru “Kyusa” na kusababisha watoto waliokuwa wanazaliwa na wageni wengine wakaitwa Wanyakyusa.

Nadharia hii inabainisha kuwa asili na chimbuko la Wanyakyusa ni eneo la Kabale kutokana na makabila mawili ya Mluguru na Mzulu na utawa ulianzia hapo.

Muunganiko wa watu kutoka pande tatu za Mashariki (Nselya), Magharibi (Abangumba), Wabungu (Abamwamba) na Wangonde (Bantebela) ndiyo asili na chimbuko la Wanyakyusa wa Kabale mwambao mwa Mlima Rungwe.

Na inasemwa kuwa hii ndiyo asili ya makabila mengine ya Wandali, Wamalila, Wasafwa, Wakagulu, Wafipa, Wabungu na wengine waishio kando kando ya milima na wenye utamaduni, mila na desturi moja.

Mavazi ya asili ya Wanyakyusa

Kwa upande wa mavazi, Wanyakyusa walikuwa wanavaa mavazi yaliyojulikana kama “Lyabi”. Haya ni mavazi ya kwanza kwa kabila hili yakivaliwa enzi za utumwa. Ni mavazi yaliyofunika maeneo ya siri pekee, na kwa wale ‘waheshimiwa’ walivaa vazi lililoitwa “kikwembe” au “kilundo”.

Mavazi haya yalivaliwa kwa mtindo kama lubega, ndiyo yaliyomtambulisha na kumtofautisha mhusika mbele ya jamii.

Ngoma ya asili ya Wanyakyusa

Kuna aina nyingi za ngoma na nyimbo ambazo Wanyakyusa wamekuwa nazo. Kwa mfano kuna ngoma ya ‘indingala ja lukino’, ‘ipenenga’, ‘ing’oma’, ‘amaghosi’, ‘ikiboota’, ‘ikimele’ na ‘akapote’, kwa kutaja baadhi.

Wana nyimbo ambazo huimbwa katika shughuli mbalimbali za kijamii, kiuchumi, kiutamaduni na kisiasa. Nyimbo hizo ni kama vile ‘isombola’, ‘indendi’, ‘ikulumba’, ‘akapote’ na ‘ikwengima’.

Nyimbo za ngoma zilikuwa na umuhimu wake katika jamii ya Wanyakyusa tangu zamani kwani lengo kuu la nyimbo hizo lilikuwa ni kuelimisha na kuburudisha jamii.

Ngoma iliyokuwa inachezwa sana na Wanyakyusa enzi hizo ilikuwa ni ya kuchezea mikuki na mara nyingi ngoma hiyo ilikuwa ikichezwa wakati wa msiba.

Lakini ngoma za kawaida zilizokuwa zinachezwa pasipo kutumia mikuki na wakati wa sherehe na shughuli nyingine ni “ipenenga”. Ngoma hii mara nyingi ilikuwa inachezwa na watu ‘wastahiki’ tena kwa madaha na maringo ya hali ya juu. Hata machifu walikuwa wakiicheza sana ngoma hii.

Chakula cha asili cha Wanyakyusa

Chakula kikuu na ambacho Mnyakyusa angeonekana kuwa amemkirimu mgeni, si kingine bali ni ndizi zinazomenywa na kupikwa, maarufu kama ‘mbalaga’.

Mnyakyusa halisi kama atakula chakula lakini akakosa mbalaga hujiona kama bado hajakamilisha mlo ingawa siku hizi kuna mabadiliko fulani, ambapo wengi hupendelea ugali na wali, lakini bado asili ya chakula chao hawawezi kuibadilisha kamwe.

Na ni lazima chakula kama kande (chakula chenye mchanganyiko wa mahindi na maharage) kipikwe kwenye tukio la msiba uwao wowote, kama shughuli za msiba zitakwisha pasipo kupikwa kande, msiba huwa haujakamilika, hata kama wafiwa ni watu wenye kujiweza kifedha zaidi lakini ni lazima kande zitapikwa japo kiasi.

Makala haya yametokana na vyanzo mbalimbali vya habari.

0685 666964 au [email protected]

Join our Newsletter