Uko hapa: NyumbaniHabari2021 11 19Article 572764

Habari za Afya of Friday, 19 November 2021

Chanzo: mwananchidigital

Wapendekeza CHWs watumike uzazi wa mpango

Wapendekeza CHWs watumike uzazi wa mpango Wapendekeza CHWs watumike uzazi wa mpango

Wadau sekta ya afya wameshauri watoa huduma ngazi ya jamii (CHWs) watumike kusaidia huduma za uzazi wa mpango kama moja ya kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi ikiwemo watoto wachanga wanaofariki mara baada ya kuzaliwa.

Hayo yamesemwa leo Ijumaa Novemba 19, 2021 katika mdahalo uliohusu masuala ya afya ya uzazi na umuhimu wa matumizi ya uzazi wa mpango ikiwa ni sehemu ya mkutano wa mwaka wa kisayansi wa huduma za afya ya uzazi na mtoto.

Wamesema uwepo wa huduma za karibu kutoka kwa wataalamu ngazi za chini utasaidia kinamama kuwa wawazi lakini pia kushirikisha wanaume wengi kutokana na wahudumu hao kuwa karibu na jamii.

Mganga Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Dk Nyembea Hamad amesema watoa huduma ngazi ya jamii wao wanaishi na jamii na kila kijiji au mtaa huwachagua kwa kuangalia sifa wanazopenda wao kulingana na utamaduni wa sehemu husika.

“Hivyo kuwatumia kwa ajili ya huduma za uzazi wa mpango itasaidia huduma kupatikana karibu na walipo kwani kila kijiji au mtaa wanakuwepo wawili wawili na wanaweza wakawa wanakuwa na njia za uzazi wa mpango nyumbani hasa zile ambazo hazihitaji utaalamu mkubwa,” ameshauri Dk Hamad.

Wadau hao wamesema bado kuna baadhi ya maeneo ikiwemo mkoani Katavi bado kuna wagonjwa wa fistula hivyo suala ya elimu kuhusu uzazi salama ni muhimu hivyo lazima waangalie nini kinafanyika kuhakikisha kinamama wengi wanaondokana na tatizo hilo.

Wadau mbalimbali mashirika yasiyo ya kiserikali wanaoendesha miradi ya uzazi wa mpango, wamesema tayari Serikali imeonyesha msimamo wake kutumia njia za uzazi wa mpango na hilo linawapatia wao nguvu kubwa kutekeleza miradi iliyopo kwa kufuata mwongozo wa nchi.

Maneja mauzo upande wa mashirika kutoka T-Marc Tanzania, Lilian Erasmus amesema matumizi ya njia za uzazi wa mpango ni muhimu kwa sasa kutokana na malengo endelevu ya dunia yaliyopangwa na Tanzania kama nchi lazima waikamilishe.

“Kwa sasa Serikali imeonyesha msimamo wake hivyo mashirika nasi wazalishaji wa condom, vidonge vya uzazi wa mpango tunahamasika na tunaona ajenda hii imepata mwitikio mkubwa hivyo tunaungana na Serikali kufanya kazi kwa pamoja,” amesema Erasmus.