Uko hapa: NyumbaniHabari2021 06 07Article 541411

xxxxxxxxxxx of Monday, 7 June 2021

Chanzo: www.habarileo.co.tz

Wasomi, wanasiasa watoa mbinu kilimo kivutie vijana

WASOMI, wanasiasa na wadau wa kilimo wametaja sababu za vijana kukwepa kilimo huku wakitoa mbinu za kuifanya sekta hiyo iwavutie na kuwafanya washiriki kikamilifu na kufaidika nayo.

Makama wa Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sokoine Cha Kilimo (SUA), Profesa Raphael Chibunda, amesema kama mbinu za kilimo hazitabadilika ili kitajirishe wakulima, sekta hiyo haiwezi kuwa na mvuto kwa vijana.

Chibunda alisema ofisini kwake Morogoro alipozungumza na HabariLEO kuwa, taifa linapaswa kuacha kilimo cha kutegemea mvua, lizingatie cha umwagiliaji, zitumike zana za kisasa na kuwe na uhakika wa masoko.

“Naamini kwa kufanya hivyo vijana wengi wataingia katika kilimo kwa sababu kilimo kinaweza kikamtoa mtu katika lindi la umasikini na kuwa tajiri mkubwa kama kazi nyingine zilivyo," alisema Profesa Chibunda.

Alisema kilimo bado ni msingi wa uchumi wa nchi kwa kuwa asilimia 70 ya Watanzania wanakitegemea kuendesha maisha yao.

Mhadhiri SUA, Dk Philbert Ninyondi, alisema kilimo hakina mvuto kwa vijana kwa kuwa wanaishi kwenye dunia ya kisasa, lakini sekta hiyo inaendeshwa kizamani.

“Kama kilimo kipo kwenye dunia ya enzi za babu kinawezaje kuwavutia. Nani anavutiwa kutumia usafiri wa punda au ngamia. Vijana wangapi wanavutiwa na hata usafiri wa baiskeli. Kama kilimo cha Tanzania kingekuwa cha kisasa, kimuundo mbinu na teknolojia, vijana wengi kama si wote wangekimbilia huko,” alisema Profesa Ninyondi.

Alilieleza gazeti hili kuwa, wasomi katika nchi zilizoendelea wanawekeza kwenye kilimo kinachotumia teknolojia ya kisasa.

“Kilimo cha jembe ni mbegu za mababu ni cha kujikimu tu. Vijana wanataka maisha mazuri, wanataka kilimo cha biashara, kilimo kinacholipa,” alisema Dk Ninyondi.

Akaongeza: “Fikiria msomi akimaliza SUA, ashike jembe alime kwa sababu tu ana ujuzi ni kujifurahisha. Bora akaendesha bodaboda akawa na uhakika wa anachopata.”

Dk Ninyondi alisema taifa linahitaji diplomasia ya kilimo ili lipate teknolojia itakayovutia vijana kwenye kilimo na pia litafutwe soko la uhakika la mazao.

Alisema wakati umefika wa kutoa fursa kwa kilimo, kiwe kama biashara nyingine ambapo mkulima ataruhusiwa kutafuta soko na bei nzuri popote, diplomasia itumike kuweka mazingira na kulinda maslahi ya taifa kama biashara nyingine.

Dk Ninyondi pia alisema vijana hawana budi kuhamasishwa kuingia kwenye kilimo na kutumia ujuzi walionao kama yatakuwepo mashamba makubwa ya umma yenye miundombinu inayoruhusu kukodiwa ikiwa ni pamoja na kupata mitambo ya kukodi na kuzalisha.

Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Agostino (SAUT), Profesa Costa Mahalu alisema vijana hawapendi kilimo kwa kuwa katika jamii za Kiafrika mkulima mdogo alionekana kuwa masikini.

Mahalu alilieleza HabariLEO kuwa vijana wanaamini mijini kuna fedha nyingi na maisha ni mazuri kuliko vijijini, hivyo wengi wamekimbilia mjini ili kutafuta utajiri.

“Wanaamini wakiwa na fedha wao ni matajiri na kuwa wanaweza kumudu aina yoyote ya maisha na wanatafuta fedha kwa kila njia/biashara isipokuwa tu kwenye kilimo bila kufahamu kuwa kilimo ndicho chanzo kikuu cha maisha,”alisema.

Akaongeza: “Uelewa wa kilimo kwa vijana wetu ni ile hali ya umasikini wanayoiona vijijini bila kuelewa kwamba, kilimo ni chanzo cha utajiri ulimwenguni pote na kwamba, kilimo kinahitaji umakini mkubwa, nguvu nyingi na uvumilivu wa hali ya juu.”

Profesa Mahalu alisema vijana wanabeza kilimo kwa sababu hakiwatajirishi haraka na wao wanataka utajiri wa haraka jambo alilosema si sahihi.

“Hii si kazi ndogo na hasa wakati huu ambapo mitandao mingi ikithamini upatikanaji wa fedha haraka kwa ku-promote (kuchochea) shughuli nyingine nyingine bila kuinua umuhimu wa kilimo,” alisema.

Mkulima wa zao la mahindi katika eneo la Kiegea mkoani Morogoro, Flora Msangi, alisema kilimo kinakatisha tamaa kwa kuwa bado ni cha kizamani na kinachotegemea mvua.

Katibu wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Kanda ya Ziwa Victoria (Mwanza, Geita na Kagera), Zacharia Obadi, alisema kilimo hakina mvuto kwa vijana kwa kuwa ni cha kizamani hivyo hawaoni tija ya kulima.

“Vijana hawa kwa sasa wanapeana elimu kupitia facebook, twiter na whatsApp, vijana wengi waliohitimu vyuo vikuu na wale ambao hawakwenda vyuoni wanavutiwa sana na kilimo, lakini kwa bahati mbaya kwa sababu kilimo kimekosa faida; hakina tija,” alisema

Katibu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Morogoro, Alexandrina Katabi, alisema baadhi ya vijana wanaona kilimo si ajira kwao, hivyo lazima kuwe na mkakati kiwe na mvuto kwao.

Mkurugenzi wa Shirika la Wote Sawa la jijini Mwanza, Angel Benedicto, alisema ili vijana wapende kilimo jamii iondokane na dhana kuwa kilimo ni adhabu na pia, viongozi wasisubiri kustaafu ndio waanze kulima.

“Serikali itenge maeneo maalumu yenye tija yatakayotumiwa na vijana kwenye kilimo, ikiwemo mikopo yenye riba nafuu, mfano mkulima anachukua mkopo anatumia pesa zote kutokana na kukosa soko, kibaya zaidi hawezi kurudisha hata mtaji aliowekeza,” alisema.

Mkurugenzi wa Utafiti na Sera wa Taasisi ya Governance Link, Donald Kasongi, alisema ili vijana wapende kilimo ni muhimu kuangalia taswira ya hali ya maisha ya mkulima nchini.

“Kwa sababu ya taswira ya mkulima, kuwa ni mtu wa kijijini na haonyeshi mabadiliko chanya, vijana wanaonakuwa kilimo ni kitu ambacho hakiwezi kubadilisha maisha yao,” alisema na kuongeza kuwa, ni muhimu yajengwe mazingira ya kumwezesha kijana kupata mkopo katika taasisi za fedha zikiwamo benki kwa masharti na riba nafuu.

Mkurugenzi wa Huduma wa Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC), Julian Mutunzi, alisema ili vijana wapende kilimo ni lazima yaandaliwe mazingira rafiki ya kisera na miundombinu ili kiwe cha kibiashara.

Mutunzi akiwa mkoani Geita alisema vijana wanapenda kuona matokeo haraka, hivyo ili wavutiwe kwenye kilimo, lazima yaandaliwe mashamba darasa yatakayotumika kama vituo vya mafunzo yao.

“Tunajua kuwa sehemu nyingi za vijijini vijana wanalima, hivyo hatuwezi kusema kwamba vijana hawalimi kabisa, lakini tunazungumuzia kile kilimo cha biashara, kilimo ambacho kitakuwa sehemu ya ajira na maisha yao na kwa njia ya mashamba darasa vijana wataweza kuendeleza kilimo cha biashara, na kuiona ni sehemu ya ajira kwao,” alisema.

Katibu wa CCCM wa Wilaya ya Kahama, Emmanuel Mbamange, alisema vijana wengi wanafanya biashara ndogondogo badala ya kulima kwa kuwa kazi hiyo inaonekana kuwa ni ya kimasikini.

Mbamange alisema kilimo kimekosa tija na ni cha kubahatisha hivyo, ni ngumu kupata mitaji kwa kuwa pia hakuna soko la uhakika la mazao.

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga, Ngassa Mboje, alisema kilimo hakiwavutii vijana kwa kuwa ni cha kubahatisha hasa kwa kuwa kinategemea mvua.

“Sababu nyingine kuu ya vijana kutopenda kilimo ni usomi walionao na kuona ni kazi ya kimasikini na kujikita kutafuta ajira, lakini asiye na elimu ataona kinamfaa siku zote hana pa kukimbilia,” alisema Ngassa.

Mtaalamu wa kilimo na mifugo, Abdul Kafuku, alisema kilimo kinalipa lakini lazima ufahamu unalima nini na soko liko wapi.

Ofisa Kilimo Mstaafu, Aithan Chaula, alisema vijana wanatakiwa kuaminishwa kuwa kwa uhalisi kuwa kilimo ‘kinalipa.’

“Wanajifunza kutoka kwa wazee, anaona wazazi wake tangu wameanza kulima hakuna mabadiliko, wanaona kama adhabu hakiwezi kumtoa mtu, ndio maana vijana wengi wamejiingiza kwenye kazi za kuendesha pikipiki kazi ambayo itampa fedha za haraka haraka,” alisema Chaula.

Chaula ambaye pia ni Katibu Mtendaji wa Shirika la la Agriculture Seeds Production Association (DASPA), alisema ili kilimno kiwe na mvuto hususan kwa vijana ni muhimu mfumo wa sekta hiyo uwe wenye kueleweka na wa uhakika.

“Wakati mwingine serikali ifike mahali iingize mkono wake kuwasaidia vijana wanaowekeza kwenye kilimo,” alisema

Imeandikwa na Agnes Haule (Morogoro), Lucy Ngowi (Dar es Salaam), Nashon Kennedy (Mwanza), Yohana Shida (Geita), Kareny Masasy (Shinyanga) na Sifa Lubasi (Dodoma).

Join our Newsletter