Uko hapa: NyumbaniHabari2022 01 14Article 585847

Habari za Mikoani of Friday, 14 January 2022

Chanzo: www.tanzaniaweb.com

Watatu wafariki dunia kwa kufukiwa na kifusi Arusha

Watatu wafariki dunia kwa kufukiwa na kifusi Arusha Watatu wafariki dunia kwa kufukiwa na kifusi Arusha

Watu watatu wamepoteza maisha mara baada ya kufukiwa na kifusi kwenye machimbo ya mchanga mwekundu maarufu kama 'moramu' yaliyopigwa marufuku kutumika katika eneo la Mlimani CCM, Kata ya Murieti Jijini Arusha.

Kabla ya kukatika gema na kuanguka kwenye machimbo hayo, ndani yake kulikuwa na watu watano waliokuwa wakiendelea na shughuli za uchimbaji wa mchanga huo.

Taarifa kuhusu ajali hiyo zilithibitishwa jana na Mkuu wa Wilaya ya Arusha, Said Mtanda, muda mfupi baada ya kutembelea eneo hilo la machimbo ya Mlima CCM kwa ajili ya kusimamia kazi ya ukoaji.

“Nitoe pole kwa wafiwa kutokana na tukio hili, lakini niseme kwamba serikali inapokataza kufanya shughuli za uchimbaji katika maeneo kama haya, huwa inaona kabisa kuwa yatatokea majanga kama haya.

Zaidi Mtanda alisisitiza, “Naelekeza kuanzia sasa Jeshi la Polisi, Tume ya Madini na Baraza la Taifa la Usimamizi na Uhifadhi wa Mazingira (NEMC) kuweka doria katika eneo hili pamoja na maeneo yote yaliyopigwa marufuku shughuli za uchimbaji madini ya mchanga.

“Hasa kule Moshono, na wale wote watakaobainika kuendeleza shughuli hizi wafikishwe kwenye vyombo vya sheria.” Alipoulizwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Kamishna Msaidizi, Justine Masejo, alisema watu hao walifariki dunia Januari 12, mwaka huu.

Kutokana na kuharibika kwa miili ya watu hao, Mtanda alimwagiza Mkuu wa Polisi wa Wilaya ya Arusha (OCD), kuruhusu miili ya marehemu itakayotambuliwa kuchukuliwa na ndugu zao ili kwenda kuizika.

Mganga Mfawidhi wa Kituo cha Afya cha Murieti, Hamis Balewa, alisema walipokea miili mitatu ya watu hao juzi jioni majira ya saa 10:30 jioni ikiwa imeharibika vibaya maeneo ya kichwani na mmoja eneo la kifua.

“Miili tuliyoipokea ni ya vijana wa kiume na wanaonekana wakiwa na umri mdogo ambao ni kati ya miaka 23 na 24, ikiwa imeharibika sehemu za kichwani kutokana na kuangukiwa na gema iliyokuwa imebeba mawe na udongo " alisema Dk. Balewa.

Alipotafutwa Mwenyekiti wa Wachimbaji Moramu, Peter Kachema, alisema walikuwa vijana watano wakichimba eneo hilo, kwamba ngema hiyo ilipoanguka walifanikiwa kukimbia watu wawili, huku watatu wakisalia ndani ya shimo hadi umauti ulipowakuta.