Uko hapa: NyumbaniHabari2021 07 02Article 544975

Habari Kuu of Friday, 2 July 2021

Chanzo: www.habarileo.co.tz

Watendaji wa serikali wapewa maagizo 10

Watendaji wa serikali wapewa maagizo 10 Watendaji wa serikali wapewa maagizo 10

WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa ametoa maagizo 10 kwa watendaji wa serikali likiwemo la kusimamia posho za madaraka, kumalizia ujenzi wa madarasa na kusimamia mifumo ya kilimo.

Majaliwa alitoa maagizo hayo Dodoma jana katika hotuba ya kuahirisha mkutano wa tatu wa Bunge la 12.

Alisema, mawaziri wanapaswa kusimamia vizuri mpango wa bajeti ya serikali ili kutumika inavyotakiwa na kwamba, Tamisemi wanapaswa kusimamia posho za madaraka kwa watendaji wa kata na vijijini na mitaa.

Alizitaka mamlaka za serikali za mitaa zitenge maeneo maalumu kwa ajili ya vijana, wafanyabiashara, wanawake na watu wenye ulemavu na kuwapa elimu katika kuwashirikisha kubainisha maeneo ya kufanyia shughuli hizo.

Majaliwa pia alizitaka mamlaka za serikali za mitaa zikamilishe maboma ya shule za msingi, sekondari, zahanati, na zianze ujenzi wa shule za wasichana zinazofundisha masomo ya sayansi ambayo tayari wamepelekewa fedha.

Aliitaka Wizara Mawasiliano na Teknolojia ya Habari ishirikiane na Tamisemi kukamilisha mpango anuwai wa makazi ili kurahisisha utambuzi wa anuani za makazi ya wananchi.

“Nitoe mwito kwa Watanzania kutumia vizuri mitandao ya kijamii kama chachu ya kuibua na kukuza fursa za kiuchumi sambamba na kumarisha mawasiliano katika huduma mbalimbali katika jamii”alisema Majaliwa.

Majaliwa alizitaka wizara na taasisi za serikali ziimarishe huduma za uwekezaji kwa wafanyabiashara waliojitika katika huduma za mitandao na wasimamie changamoto za kisheria na kanuni.

Aliielekeza Wizara ya Kilimo iendelee kusimamia mifumo ya ununuzi wa mazao kwa stakabadhi ghalani na kwa mikoa ambayo elimu bado haijatolewa vya kutosha, itolewe kuhusu faida ya mfumo huo.

Majaliwa aliitaka Wizara ya kilimo isimamie mfumo wa ununuzi wa pembejeo kwa pamoja na ihakikishe inamaliza changamoto za wakulima ili wapate pembejeo mapema.

Aliagiza wakulima wa pamba wasikatwe gharama za pembejeo kwa sababu zipo kwenye mjengeko wa bei.

Kwa upande wa tumbaku, wizara ya kilimo na wizara ya fedha kukamilisha mazungumzo na mnunuzi wa tumbaku hususani kipindi hiki wakati soko la zao linaimarika katika soko la dunia. Tatuteni masoko ya tumbaku ya moshi ili wakulima wa zao hilo wapate soko la uhakika.