Uko hapa: NyumbaniHabari2021 07 04Article 545296

Habari za Afya of Sunday, 4 July 2021

Chanzo: www.habarileo.co.tz

Watoa huduma wanaoghushi madai ya NHIF kukiona -Gwajima

Watoa huduma wanaoghushi madai ya NHIF kukiona -Gwajima Watoa huduma wanaoghushi madai ya NHIF kukiona -Gwajima

SERIKALI imeonya watoa huduma wanaojihusisha na udanganyifu katika uchakataji wa madai ya huduma za matibabu wanayoyawasilisha Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) na kuwataka waache mara moja.

Aidha baadhi ya watoa huduma ambao walishawakilisha madai kwa Mfuko yenye udanganyifu na baadaye yakagundulika, wajiandae kurejesha fedha kwa kuwa serikali haiwezi kukubaliana na vitendo hivyo vyenye kulenga kudhoofisha huduma za afya.

Onyo hilo lilitolewa hivi karibuni jijini Dodoma na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto, Dk Dorothy Gwajima wakati akizindua Bodi ya Wakurugenzi ya NHIF pamoja na uzinduzi wa maadhimisho ya miaka 20 ya NHIF tangu kuanzishwa kwake.

“Wote waliofanya udanganyifu katika madai ya Mfuko huu au kutumia taaluma zao kwa ubadhirifu naomba niwape taarifa mapema kwamba wajipange kuzirejesha fedha hizo na kwa wale ambao bado wanaendelea na vitendo hivi ni bora waache mara moja kwa kuwa tukibaini hatua kali dhidi yao zitachuliwa na katika hili niseme wazi kabisa kuwa nitalishughulikia mwenyewe ninachohitaji ni ushahidi tu na Mkurugenzi Mkuu nataka kila robo mwaka unipatie taarifa ya malipo yanayofanywa ili tuweze kujenga huu uaminifu ,” alisema Gwajima.

Aliagiza Bodi ya Mfuko kuhakikisha inasimamia na kuitangaza Sera ya Mfuko ya utoaji wa taarifa kwa siri wananchi wajue wanatoaje taarifa hizo ambazo zinalenga kukomesha udanganyifu wa kihuduma .

Akizungumzia uboreshaji wa huduma katika vituo vya kutolea huduma, alisema kuwa Serikali imefanya jitihada kubwa za kuhakikisha dawa na vifaa tiba vinapatikana lakini pia akatumia nafasi hiyo kuwataka watoa huduma kutumia fursa ya mikopo ya vifaa tiba na ukarabati wa majengo inayotolewa na Mfuko.

Katika hatua nyingine, Waziri Gwajima alizungumzia utekelezaji wa suala la Bima ya Afya kwa Wote ambapo aliuhakikishia umma kuwa Muswada wa sheria unatarajiwa kuwasilishwa bungeni Septemba mwaka huu na kwa upande wa wizara yake, maandalizi yote yameshakamilika.

Alitoa maagizo kwa Bodi mpya ya NHIF kuhakikisha inasimamia uendelevu na uimarishaji wa Mfuko pamoja na kuhakikisha wananchi walioko katika maeneo ya vijijini wanafikiwa na huduma hizo.

Mwenyekiti wa Bodi ya NHIF, Juma Muhimbi, alisema kuwa yeye na bodi yake watahakikisha wanafanya kazi kwa kuzingatia matarajio makubwa ya Serikali na wananchi waliyonayo katika Mfuko huo.

Mkurugenzi Mkuu wa NHIF, Benard Konga akizungumza katika hafla hiyo alisema lengo la Mfuko ni kuhakikisha unasogeza huduma zake kwa wananchi ili wasipate changamoto yoyote katika kupata huduma za bima ya afya.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi aliyemaliza muda wake, Spika Mstaafu, Anne Makinda alishukuru Mfuko na Wizara kwa kushirikiana na bodi aliyoiongoza kwa kazi kubwa iliyofanywa na bodi yake ikiwemo uanzishwaji wa Vifurushi vya Bima ya Afya ambavyo vinamwezesha kila mwanachi sasa kujiunga na kunufaika na huduma za bima ya afya kwa kadri ya uwezo wake wa kuchangia.