Uko hapa: NyumbaniHabari2021 06 04Article 540928

Habari za Mikoani ya

Chanzo: www.habarileo.co.tz

Wavuliwa nyadhifa kwa uzembe meli iliyonusurika kuzama

Wavuliwa nyadhifa kwa uzembe  meli iliyonusurika kuzama Wavuliwa nyadhifa kwa uzembe meli iliyonusurika kuzama

MAOFISA wawili wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) wamevuliwa nyadhifa zao kutokana na tuhuma za kushindwa kufanyia kazi taarifa zilizohatarisha usalama wa Meli ya abiria ya MV Mbeya II iliyonusurika kuzama hivi karibuni baada ya kupigwa na dhoruba.

Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mwita Waitara aliagiza kuvuliwa nyadhifa zao alipofanya ziara juzi ikiwa ni mara ya pili kufika katika Bandari ya Kiwira iliyopo Ziwa Nyasa, Wilaya ya Kyela mkoani Mbeya.

Waitara aliwataja maofisa wanaotakiwa kuvuliwa nyadhifa zao kuwa ni pamoja na Kaimu Meneja Mkuu wa Bandari za Ziwa Nyasa, Hamisi Nyembo na Nahodha, Abdallah Mwengamno aliyeko Makao Makuu ya TPA akitaka wapangiwe kazi zingine.

Alitoa agizo hilo baada ya kufanya kikao cha pamoja na wadau wa meli za Ziwa Nyasa na kubaini kuwa maofisa hao wawili walishapewa muda mrefu taarifa za kuwepo kwa hitilafu kwenye Meli ya MV Mbeya II lakini hawakuwahi kuchukua hatua zozote ili hitilafu hizo zifanyiwe kazi na kusababisha abiria kuendelea kusafiri kwa mashaka.

“Hawa manahodha wa meli hizi baada ya kusafiri kwenda Ruvuma, waliporudi walitoa taarifa kwa maandishi na kumkabidhi huyu Mhandisi Nyembo ambaye pia alizifikisha taarifa hizo kwa nahodha Mwengano aliye Makao Makuu ya TPA, lakini hakuna hatua walizochukua na wakaruhusu chombo hiki kuendelea kufanya kazi na kuhatarisha maisha ya watu,” alisema Waitara.

“Kutokana na uzembe huo naagiza hawa waondolewe kwenye nafasi zao ili waje watu wengine tufanye kazi, serikali inachotaka sasa hivi ni watu wanaofanya kazi na kuonesha matokeo chanya na ndio maana Rais (Samia Suluhu Hassan) alibadilisha Mkurugenzi Mkuu wa TPA,” aliongeza.

Pamoja na kuwavua nyadhifa zao maofisa hao wawili, Waitara alitoa muda wa siku 14 kwa uongozi wa mamlaka hiyo kushirikiana na Mtengenezaji wa meli hiyo, Kampuni ya Songoro Marine kuhakikisha hitilafu zilizo kwenye meli ya MV Mbeya II na meli zingine zilizojengwa na kampuni hiyo zinarekebishwa na meli hizo zirejee na kuanza safari lakini kabla hazijaanza kufaya kazi lazima wasaini makubaliano maalumu.

Aidha alitoa siku 14 kwa TPA kushughulikia madai ya wafanyakazi wa bandari za Ziwa Nyasa ili wafanyakazi wafanye kazi kwa moyo kwa maelezo kuwa lengo la serikali ni kuhakikisha TPA inafika muda ambao itajiendesha kwa faida.

Pia aliagiza watendaji wa Wakala wa Huduma za Meli nchini (TASAC) kuzifanyia tathimini meli zote za abiria zinazofanya kazi ndani ya Ziwa Nyasa na kutolea taarifa ili kama kuna matatizo yarekebishwe.

Akizungumzia tatizo lililoikumba meli ya MV Mbeya II, Mkurugenzi Mtendaji wa TASAC, Kaimu Mkeyenge alisema baada ya meli hiyo kupigwa na dhoruba waliifanyia uchunguzi na kubaini ilipata madhara kwenye maeneo mbalimbali.

Mkeyenge alisema walibaini kuwa maji yaliingia kwenye mfumo wa injini na kusababisha hitilafu kwenye injini ya kulia ya meli hiyo na kwamba mawimbi yalikuwa sio ya kawaida na ndio maana maji yaliingia kwenye eneo ambalo huwa sio kawaida kufika.

Pia taa za upande wa kulia ziliharibika na hivyo kuwa vigumu meli hiyo kuonekana usiku na kwamba tatizo hilo lilisababisha ugumu hata wakati wa uokozi.

“Kwa sasa tunaahidi kufanyia kazi maagizo ya Naibu Waziri ili kuhakikisha kwamba watumiaji wa vyombo hivi wanakuwa salama wakati wote, lakini tulishafanya tathimini kabla meli haijaanza kufanya kazi na hata baada ya kuanza kazi kulikuwa hakuna tatizo ila kilichotokea ni matukio ya asili,” alisema Mkeyenge.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa TPA, Erick Hamis alisema watahakikisha wanafanyia kazi maelekezo yote na Naibu Waziri ili kuhakikisha meli hizo zinakuwa na usalama wa kutosha kwa abiria na mizigo ambayo huwa inasafirishwa.

Hamis alisema TPA ni chombo cha biashara na hivyo kitendo cha meli ya MV Mbeya II kusimama kufanya kazi ni hasara kubwa kwa mamlaka hiyo, hivyo watalazimika kufanya kazi ya kuirekebisha haraka.

Kwa upande wake, Mbunge wa Jimbo la Kyela, Ally Jumbe aliomba wananchi wa Wilaya ya Kyela kupewa taarifa sahihi za usafiri huo wa meli kwa maelezo kuwa wao ndio wanaoutumia na ni wadau muhimu.

Join our Newsletter