Uko hapa: NyumbaniHabari2021 10 11Article 562621

Habari za Afya of Monday, 11 October 2021

Chanzo: ippmedia.com

Wazee Kigoma watakiwa kujitokeza kupata chanjo ya UVIKO-19

Wazee Kigoma watakiwa kujitokeza kupata chanjo ya UVIKO-19 Wazee Kigoma watakiwa kujitokeza kupata chanjo ya UVIKO-19

MWENYEKITI wa Baraza la Wazee wilayani Kibondo mkoa wa Kigoma, Ernest Chubwa amewataka wazee wa Kijiji cha Maloregwa Kata ya Rusohoko wilayani humo kujitokeza kupata chanjo ya UVIKO-19.

Chubwa ametoa rai hiyo alipokuwa akizungumza na wazee wa kijiji hicho kwa lengo la kuwahamasisha wajitokeze kwa wingi, kutokana na kwamba, baadhi yao wanahusisha chanjo hiyo na mambo mengine, tofauti na malengo ya serikali katika kupambana na mlipuko wa ugonjwa huo.

"Wazee wenzangu, serikali haipo tayari kuwapoteza wazee kwa magonjwa, tumepewa kipaumbele kwa sababu kinga mwili zetu zimepungua nguvu kutokana na umri, tunachanja ili kuongeza kinga, tusipuuze, tusije kupata athari kubwa zaidi," alisema Chubwa.

Mratibu wa chanjo wilayani Kibondo, Malugu Malili alisema wazee na watu wenye magonjwa sugu wanapewa kipaumbele cha kupata chanjo hiyo kutokana na kukabiriwa na upungufu wa kinga mwilini hivyo kuwa katika hatari kubwa ya kupata maambukizi ya virusi vya corona.

Mzee Rashid Nzogela aliishauri serikali kupitia maafisa afya waliopo kuendelea kutoa elimu ya kina juu ya njia za kujikinga na ugonjwa huo, faida ya chanjo na malengo sahihi ya utoaji wa chanjo hiyo, kwa kuwa wazee wengi wanaamini kuwa wakipata chanjo hiyo watapoteza maisha.

“Kwanini vipumbele wapewe wazee na watu wenye magonjwa sugu na sio makundi mengine? Serikali ina mpango gani na sisi na watu wenye magonjwa sugu? ," aliuliza mzee Nzogela.