Uko hapa: NyumbaniHabari2021 06 20Article 543550

Habari Kuu of Sunday, 20 June 2021

Chanzo: www.habarileo.co.tz

Waziri Mkumbo ataka EPZA kufahamika

Waziri Mkumbo ataka EPZA kufahamika Waziri Mkumbo ataka EPZA kufahamika

WAZIRI wa Viwanda na Biashara, Profesa Kitila Mkumbo ametaka juhudi za makusudi zifanyike ili kuhakikisha shughuli za Mamlaka ya Maeneo Maalumu ya Uwekezaji kwa Mauzo ya Nje (EPZA) zinafahamika kwa umma na wadau wakiwamo wawekezaji wa ndani na nje ya nchi.

Amesema hayo katika uzinduzi wa kongamano la siku moja kuhusu ‘Uhusiano Kati ya Maeneo Maalumu ya Uwekezaji na Uchumi wa Ndani’ lililofanyika Dar es Salaam.

Katika kongamano hilo lililoandaliwa kwa ushirikiano wa EPZA na Uongozi Institute, Kitila alitaka juhudi zifanyike zaidi kuitangaza EPZA na majukumu yake ili kujenga uelewa wa watu kuhusu mamlaka hiyo na fursa zilizopo.

Alisema Rais Samia Suluhu anasisitiza umuhimu wa kuweka msukumo wa kuboresha mazingira ya uwekezaji na biashara yakiwamo maeneo maalumu ya uwekezaji na mitaa ya viwanda ili kuchochea uwekezaji katika maeneo maalumu.

“Awamu hii tutaweka mkazo mkubwa sana Kurasini… serikali imeamua kuanzia mwaka huu tutangaze eneo hilo la Kurasini (Dar es Salaam) kwa mkazo mkubwa ndani na nje ya nchi, hivyo nitoe mwito kwa wawekezaji wa ndani na nje wachangamkie eneo hili la uwekezaji la Kurasini,” alisema na kuongeza: “Tutaendelea pia Bagamoyo…”

Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa EPZA, John Mnali, alisema tangu kuanzishwa kwake mwaka 2006, EPZA imetoa leseni kwa kampuni 176.

Mnali alisema hadi kufikia Machi 2021, kampuni hizo zimewekeza mtaji wa jumla ya dola za Marekani bilioni 2.5 na kutoa ajira za moja kwa moja kwa watu 58,198.

Kwa mujibu wa Mnali, maeneo maalumu ya uwekezaji ni maeneo ya ardhi yaliyotengwa na kuendelezwa kwa kuwekewa miundombinu na huduma za msingi pamoja na sera wezeshi ili kuandaa mazingira mazuri ya uwekezaji.