Uko hapa: NyumbaniHabari2021 09 20Article 558667

Habari Kuu of Monday, 20 September 2021

Chanzo: www.habarileo.co.tz

Waziri Mkuu akataa kuzindua ofisi za Tanesco

Waziri Mkuu akataa kuzindua ofisi za Tanesco Waziri Mkuu akataa kuzindua ofisi za Tanesco

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa amekataa kuzindua mradi wa ujenzi wa Ofisi ya Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) Wilaya ya Kyerwa mkoani Kagera kwa sababu gharama zilizotumika ni kubwa kuliko aina na idadi ya majengo.

Majaliwa amekataa kufungua ofisi hiyo leo (Jumatatu, Septemba 20, 2021) akiwa katika ziara ya kukagua miradi ya maendeleo inayotekelezwa katika Mkoa huo.

“Nikiweka jiwe la msingi nitakuwa nimehalalisha majengo mengine yajengwe kwa gharama hii. Siwezi kuweka Jiwe la Msingi, gharama zilizotumika ni kubwa kuliko majengo, simamieni ujenzi wa majengo yenu na mjenge kwa kutumia mfumo wa force account”alisema Majaliwa.

Alisema Serikali ipo makini katika usimamizi wa miradi na kwamba kufanya hivyo ni maagizo kutoka kwa Rais Samia Suluhu.

Mradi huo umegharimu Sh milioni 483.42, ambapo kibanda cha mlinzi kimegharimu Sh milioni 7.03, uzio milioni 94.2, jengo la ofisi milioni 253.8 na stoo milioni 51.55.

Waziri Mkuu amesema Serikali inajenga majengo makubwa ya vituo vya afya ambayo ni jengo la mapokezi ya wagonjwa, maabara, chumba cha upasuaji, wodi ya mama na mtoto, nyumba ya daktari, chumba cha kuhifadhia maiti, kichomea taka na korido kwa gharama ya shilingi milioni 500.

Kufuatia hatua hiyo, Waziri Mkuu ameuagiza uongozi wa TANESCO uhakikishe katika miradi yake mingine ya ujenzi gharama zilingane na aina na idadi ya majengo.

Naye, Meneja Mwandamizi Usambazi wa TANESCO Makao Makuu, Mhandisi Nathanasias Nangali ambaye alisoma taarifa ya mradi huo kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, amesema mradi huo ulianza Septemba 11, 2018 na kukamilika Februari 08, 2020 kwa gharama za Sh milioni 483.4.

Amesema Mkandarasi aliyenga mradi huo ni kampuni ya M/S RK Ivestment chini ya usimamizi wa Mkandarasi mshauri TANESCO kitengo cha miliki. “TANESCO imeendelea kutumia wataalamu wake katika kusimamia na kutekeleza miradi mbalimbali ikiwemo ya ujenzi wa ofisi zake za mikoa, wilaya na vituo vya kupoza na kusambaza umeme.”

Amesema TANESCO imeendelea kutenga fedha kwa awamu kila mwaka ili kutekeleza miradi kama hiyo ambapo katika mwaka huu inaendelea na ujenzi wa ofisi za wilaya za Buhigwe-Kigoma, Ruangwa-Lindi, Urambo-Tabora, Gairo na Malinyi-Morogoro, Nanyumbu na Tandahimba-Mtwara, Kilolo-Iringa, Rorya na Serengeti-Mara, Laela-Rukwa na Meatu-Simiyu.

Akizungumzia huduma ya umeme inayotolewa katika Wilaya hiyo amesema kati ya vijiji 99 vya Wilaya hiyo vijiji 70 vinaumeme na vijiji 29 vilivyosalia vitapata huduma hiyo kupitia mradi wa REA awamu ya tatu mzunguko wa pili unaoendelea kutekelezwa.

Awali, Waziri Majaliwa alitembelea na kukagua kiwanda cha kuchenjua madini ya bati (TIN) cha kampuni ya African Top Minerals kilichopo wilayani Kyerwa ambapo alitumia fursa hiyo kumhakikishia mwekezaji huyo kwamba Serikali itaendelea kumuunga mkono.

Mkurugenzi wa kiwanda hicho, Hassan Ibar alisema mradi huo uliogharimu Sh bilioni 4 unalenga kuboresha na kukuza sekta ya madini wilayani Kyerwa na Tanzania kwa kuongeza thamani ya madini hayo katika soko la dunia, hivyo kuongeza kipato kwa wananchi.