Uko hapa: NyumbaniHabari2021 08 21Article 552847

Habari Kuu of Saturday, 21 August 2021

Chanzo: Nipashe

Waziri aijia juu TANESCO kisa kukata umeme ovyo

Waziri wa Nishati, Dr. Medard Kalemani Waziri wa Nishati, Dr. Medard Kalemani

WAZIRI wa Nishati, Dk. Medard Kalemani, amepiga marufuku tabia ya wafanyakazi wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kukata ovyo umeme kwa kisingizio kuwa gridi imehama.

Dk. Kalemani alitoa onyo hilo alipokuwa katika ziara yake ya kukagua kituo cha kufua na kupoza umeme cha Zuzu.

Alisema hivi sasa kuna tabia inayokera kwa watendaji wa Shirika hilo kukata umeme ovyo bila kutoa taarifa kwa wateja kwa kisingizio cha gridi kutoka.

“Hapa Dodoma umeme kukatia ni marufuku, lakini nashangaa juzi ulikatika ukiuliza unaambiwa eti gridi imetoka kwanini itoke na wewe upo hapo basi kuanzia leo tabia hii ikome kabisa kabla haijaondoka na mtu,” alisema Dk. Kalemani.

Alisema hivi sasa Mkoa wa Dodoma upo umeme wa kutosha kutokana na kuwapo kwa kituo cha kufua umeme cha Zuzu ambacho kikikamilika kitakuwa na uwezo wa kuzalisha Megawati za umeme zaidi ya 600.

Alisema mahitaji ya umeme kwa Dodoma hivi sasa ni Megawati 48, na yamekuwa yakipanda kila siku hivyo kituo hicho kitakuwa mkombozi kwa kuwa na umeme wa uhakika.

“Kituo hicho kinafua na kupoza umeme na kusambaza katika Mkoa wa Singida lakini baadaye kitatumia pia kupeleka nchini Zambaia na Kenya,”alisema Dk. Kalemani.

Akizungumzia matukio ya kuungua kwa vituo vya kufua na kupozea umeme nchini, Waziri huyo alisema ipo haja ya kuwekwa sawa mifumo ya kubaini tatizo linaweza kujitokeza ili hatua zichukuliwe kabla ya kutokea.

“Lile tatizo la kituo cha kupoza umeme lililotokea hivi karibuni mkoani Morogoro tayari nimeshaunda tume ili kubaini kama ilikuwa bahati mbaya au makusudi,” alisema.

Aidha, alisema ili kukomesha hali ya kuungua kwa vituo hivyo TANESCO inatakiwa kuajiri watumishi wenye uzalendo na wenye weledi katika nafasi hiyo.

“Hivi vituo ndipo umeme wote unatoka hapa tuweke watu wazalendo, wenye weledi na asiwe mlevi na nikikuta mtu mlevi yeye na aliyemwajili wote wataondoka na pia tusitumie raia wa kigeni hawa wanaweza kutuingiza chaka,” alisema Dk. Kalemani.

Naye, Meneja wa Mradi wa kituo hicho cha kufua umeme cha Zuzu, Newton Mwakifwamba, alisema mradi huo unatarajiwa kukamilika Septemba 27, mwaka huu.

“Mradi upo asilimi 98, za kukamilika na tunatarajia hadi kufikia Septemba 27, mwaka huu kuwa umekamilika na unaghalimu Dola za kimarekani milioni 53,” alisema Mwakifwamba.