Uko hapa: NyumbaniHabari2021 08 23Article 553096

Habari Kuu of Monday, 23 August 2021

Chanzo: www.habarileo.co.tz

Waziri awaonya waongoza mifumo ya umeme TANESCO

Waziri awaonya waongoza mifumo ya umeme TANESCO Waziri awaonya waongoza mifumo ya umeme TANESCO

WAZIRI wa Nishati, Dk Medard Kalemani amesema watawaondoa kazini Watumishi wa Shirika la Umeme Nchini (TANESCO) kwenye chumba cha kuendesha mfumo wa umeme kwa kutokuwa wazalendo.

Pia wataondolewa iwapo itabainika kuna hujuma zinazofanya kuungua kwa mitambo na hata kuzembea na kusababisha gridi ya taifa kutotoa umeme katika maeneo mengi ya nchi.

Pia amepiga marufuku watumishi wa chumba cha kuendesha mfumo wa umeme kuingia kazini wakiwa wamelewa.

Alisema hayo jijini hapa wakati akizungumza na waandishi wa habari baada ya kutembelea mradi wa umeme wa Zuzu.

Dk Kalemani alisema watu wanaofanya kazi kwenye chumba cha kuendesha mfumo wa umeme wanatakiwa kuwa makini.

“Hapo ndio kwenye roho ya umeme, kama mfumo wa gridi umekataa usiilazimishe hadi mitambo mingine ikaungua” alisema.

Alitaka kuwepo kwa watumishi wa kutosha kwenye chumba cha kuendesha mfumo wa umeme na wanaosimamia mitambo wawe na uzalendo na weledi.

“Ni marufuku mtumishi kuingia kazini akiwa amelewa pombe, nikija nikikuta mtu wa aina hiyo, aliyemleta na mwenyewe hawana kazi, ni sawa na mtu aliyeshika bastola analenga na kuripua,”alisema. Aidha alitaka mitambo hiyo iendeshwe na Watanzania na sio raia wa kigeni.

Aidha akizungumza kwenye eneo la mradi wa ujenzi wa upanuzi wa kituo cha kupoza umeme cha Zuzu, alitaka kulindwa kwa mfumo wa kisasa wa umeme ambao ujenzi wake umefikia asilimia 98.

Alisema ujenzi wa upanuzi wa kituo cha kupoozea umeme serikali imefadhili na kutoa dola za Marekani milioni 50 kwa ajili ya upanuzi huo.

Alisema awali kituo hicho kilikuwa na uwezo wa kuzalisha megawati 48 lakini baada ya upanuzi kitazalisha megawati 624.

“Ni umeme mwingi sana, hapa ndio kitovu, umeme huu utatoka Dodoma utaenda Singida, Shinyanga, Zambia,Namanga Kenya hili si eneo la kucheza nalo, umakini mkubwa unatakuwa,”alisema. A

lisema kumekuwa na tukio la kuunguza miundombinu ya umeme “hatutaki tukio la Morogoro lijirudie. Tumesimamisha watatu na tutasimamisha wengi zaidi kadri itakavyobidi”.

Alisema kwenye kituo hicho kipya wataweka mfumo utakaoweza kubaini lolote linaloweza kutokea. Alitaka kuwepo mfumo na hitilafu inapotokea maeneo mengine yasiathirike.

“Hiyo hali ya gridi isijirudie tutachukua hatua kali sana,” alisema. Alisema umeme upo wa kutosha hivyo hakuna sababu ya kuona umeme unakatika kwenye baadhi ya maeneo.

Pia aliwataka wananchi kuendelea kuchangamkia fursa ya kuunganishiwa umeme kwani Tanzania ni mfano kwa nchi ya Afrika katika kusambaza umeme.

Kwa upande wake, Msimamizi wa kituo hicho, Newton Mwakifwamba alisema mradi huo una thamani ya dola za Marekani milioni 53 na umekamilika kwa asilimia 98.