Uko hapa: NyumbaniHabari2021 11 19Article 572761

Habari Kuu of Friday, 19 November 2021

Chanzo: www.tanzaniaweb.com

Waziri wa Sheria kafunguka kuhusu uimara wa katiba ya Tanzania

WAZIRI wa Katiba na Sheria, Profesa Palamagamba Kabudi WAZIRI wa Katiba na Sheria, Profesa Palamagamba Kabudi

WAZIRI wa Katiba na Sheria, Profesa Palamagamba Kabudi amesema ndani ya miaka 60 ya Uhuru, taifa limeidhihirishia dunia ukomavu wa kisiasa na umadhubuti wa Katiba. Alisema hayo jana jijini Dodoma wakati akielezea mafanikio katika sekta ya Katiba na sheria ndani ya kipindi cha miaka 60 ya Uhuru.

Alisema Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imepitia mabadiliko na imesaidia kuivusha nchi katika mambo mengi na kuendelea kuwa na amani na utulivu. Alisema Katiba ya kwanza iliandaliwa na wakoloni na ikatumika kwenye uchaguzi wa mwaka 1960, ambapo kila jimbo wananchi walipiga kura kumchangua mwakilishi wa wazungu, Waasia na Waaafrika.

Profesa Kabudi alisema mwaka 1962, Jamhuri ya Tanganyika iliandika Katiba ya pili baada ya ile ya Mwingereza. Alisema mwaka 1964 iliandaliwa Katiba ya Muungano baada ya Tanganyika na Zanzibar kuungana na mwaka 1965 iliandaliwa Katiba yenye lengo la kuuimarisha. Profesa Kabudi alisema mwaka 1977 ikapatikana Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambayo mpaka sasa imefanyiwa mabadiliko mara 14.

Alisema mabadiliko ya kwanza yalifanyika mwaka 1979 ili kuiingiza Mahakama ya Rufaa kwenye Katiba ikiwa ni baada ya kuvunjika iliyokuwa Jumuiya ya Afrika Mashariki mwaka 1977. Alisema mabadiliko ya pili yalifanyika mwaka 1980 kupunguza kero za Muungano na mwaka 1982 yalifanyika tena kwa ajili ya kuboresha mfumo wa uteuzi wa wakuu wa mikoa.

Profesa Kabudi alisema mwaka 1984 yalifanyika mabadiliko mengine ambayo yalikuwa ni kuandika upya Katiba hiyo. “Mabadiliko yalilenga kuweka ukomo wa Rais kuwa vipindi viwili vya miaka mitano mitano hasa ikizingatiwa ndio kipindi ambacho Rais wa Kwanza Hayati Juliusi Nyerere alikuwa anaelekea kung’atuka.” alisema.

alisema mabadiliko hayo pia yalifanya kuongeza sura ya haki za binadamu na kuingiza tamko la haki za binadamu kuwa sehemu ya Katiba. Alisema mabadiliko ya sita na saba yalifanyikwa mwaka 1990, ambayo yalichangia kuanzishwa kwa Tume ya Uchaguzi, kuanzishwa vyama vingi vya siasa na kueleza utaratibu wa kumpata mgombea katika kiti cha urais wa Zanzibar.

Profedsa Kabudi alisema mabadiliko ya nane yalifanyika mwaka 1992 yakiweka utaratibu wa vyama vingi na kuweka utaratibu wa wabunge wa viti maalumu kufikia asilimia 15 na viti vitano vya Baraza la Wawakilishi.

“Pia kuiwajibisha serikali ndani ya Bunge kwa kupiga kura ya kutokuwa na imani na Waziri Mkuu, pia vifungu vya kuchukua pindi ikidhidhirika Rais amekiuka Katiba. Na pia iliweka utaratibu wa madiwani kuchaguliwa siku moja na wabunge na Rais,” alisema.

Profesa Kabudi alisema mwaka 1994 yalifanyika mabadaliko ya 14 ya kuweka nafasi ya mgombea mwenza na kuondokana utaratibu na nafasi ya moja kwa moja ya Rais wa Zanzibar na Waziri Mkuu mmoja wao kuwa Makamu wa Kwanza wa Rais au Makamu wa Pili wa Rais kwa kuzingati Rais anatoka upande upi wa Muungano.

mabadiliko mengine ni ya kumpa nafasi Makamu wa Rais kushika nchi endapo Rais aliyepo madarakani amefariki dunia au kushindwa kutekeleza majukumu yake. Profesa Kabudi alisema mwaka 2005 yalifanyika mbadiliko ya 13 kwa kuweka mfumo wa mshindi kutangazwa kwa kupata kura nyingi zaidi ya mwenzake badala ya kutakiwa kufikisha zaidi ya asilimia 51 ya kura, kutoa fursa kwa Rais kuteua wabunge 10 na kuongeza nafasi za viti maalumu kufikia asilimia 30.