Uko hapa: NyumbaniHabari2021 07 18Article 547381

Habari Kuu of Sunday, 18 July 2021

Chanzo: www.habarileo.co.tz

Wizara imewaza vema mikopo upimaji ardhi, hili lisichelewe

Wizara imewaza vema mikopo upimaji ardhi, hili lisichelewe Wizara imewaza vema mikopo upimaji ardhi, hili lisichelewe

JUZI Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Wiliam Lukuvi akizungumza katika kikao kazi na viongozi wapya wa mkoa wa Dar es Salaam, alisema serikali imeingia mkataba na benki ya NMB ili kutoa mikopo kwa wananchi wapimiwe maeneo yao kwa pamoja.

Mikipo hiyo ni kiasi kisichozidi Sh 150,000 na utaratibu ni mkopaji kupatiwa hati baada ya kupimiwa atakapomaliza deni lake.

Utaratibu huu kwangu nauona kama mkombozi kwa mengi. Kwanza utaokoa muda hasa kutokana na baadhi ya watu kuchelewa kulipa gharama za upimaji miradi inapotekelezwa katika mitaa yao. Pili itaondoa wasiwasi wa fedha kuliwa au kupotea kwa kuwa mfumo wa usimamizi utazihusu wilaya husika moja kwa moja.

Ni ukweli usiopingika kwamba, miradi katika maeneo mengi ya Dar es Salaam na kwingineko nchini, imesimama kutokana na kusuasua kwa kampuni zinazoitekeleza, huku ikiwaacha wananchi njia panda pasi na kujua hatima ya kupata hati zao.

Dar es Salaam ni mkoa mmoja wapo wenye changamoto nyingi za upimaji ardhi. Zipo kampuni zimekula hela za watu bila kukamilisha upimaji na kwingine kamati za ardhi zilizoundwa na wananchi zimeshindwa kusimamia zoezi hilo na kusababisha miradi hiyo kusambaratika au kutokukamilika.

Ikiwa sasa rungu wamepewa viongozi wa wilaya wakiwemo wakuu wa wilaya kuhakikisha kampuni hizo zinakamilisha kwa wakati upimaji na kusimamia malipo ya upimaji na hati, ni wazi miradi mingi inaweza kurejeshwa na katika muda mfupi ikakamilika na wananchi kupata hati kwa ajili ya kuzitumia kwa shughuli nyingine za kiuchumi ikiwamo mikopo.

Nampongeza sana Waziri Lukuvi na wizara yake kuliona hili, wananchi wana matumaini kuwa kazi inaendelea tena kwa kasi kubwa, hivyo kauli hii sasa inasubiriwa kwa hamu kuingia katika utekelezaji na si kuishia katika makabrasha maofisini.

Wakuu wa wilaya wahakikishe miradi iliyosimama kama katika eneo la Serikali ya Mtaa wa Mshikamano, Mbezi Luis, inaendelea mbele kwa wananchi ambao hawajawekewa mawe, wawekewe na waliowekewa hatua za kupata hati zifuate ili kurejesha matumaini mapya ya wananchi kwa serikali yao.