Uko hapa: NyumbaniHabari2021 06 17Article 543157

Habari Kuu of Thursday, 17 June 2021

Chanzo: www.habarileo.co.tz

Wizara kuifanya Tanzania kitovu cha mawasiliano

Wizara kuifanya Tanzania kitovu cha mawasiliano Wizara kuifanya Tanzania kitovu cha mawasiliano

WIZARA ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari imesema Tanzania inajipanga kuwa kitovu cha mawasiliano Afrika Mashariki na Kati kupitia mkongo wa taifa.

Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dk Faustine Ndugulile alisema jana jijini Dodoma kuwa serikali imetumia zaidi ya Sh bilioni 677 kujenga mkongo huo.

Dk Ndugulile alisema hadi sasa zimejengwa kilometa 8,319 katika mikoa yote 26 na wanakusudia katika mwaka ujao wa fedha waanze kujenga kilometa 1,880 ili wilaya zote ziunganishwe kwenye mkongo huo.

Aliwaeleza wahariri wa vyombo vya habari na wadau wa wizara hiyo kuwa wanakusudia nchi iwe na kilometa 15,000 za mkongo huo ifikapo mwaka 2025.

Dk Ndugulile alisema mawasiliano ya mkongo yamefikishwa kwenye nchi zote zinazoizunguka Tanzania na hivi sasa kuna kazi inafanyika kuiunganisha Tanzania na Msumbiji kwa kujenga kilometa 70 kupitia Mtambaswala.

Alisema pia unafanyika upembuzi yakinifu wa kuiunganisha Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Congo(DRC) kwenye mkongo wa taifa.

Dk Ndugulile alisema hadi sasa zaidi ya asilimia 90 ya nchi imefikiwa na mawasiliano ya teknolojia ya kawaida ya 2G, asilimia 66 inapata mawasiliano ya intaneti hadi Aprili mwaka huu laini milioni 53 za simu zilikuwa zimesajiliwa, zaidi ya laini milioni 29 nchini zinatumia intaneti.

Alisema wamepewa majukumu ifikapo mwaka 2025 mkongo wa taifa uweze kufika zaidi ya asilimia 80 ya nchi na mawasiliano ya intaneti na asilimia 70 ya huduma za serikali zitolewe kupitia Tehama.

Dk Ndugulile alisema wakati wowote kuanzia sasa watatangaza zabuni kwa ajili ya kupeleka mawasiliano kwenye maeneo ya pembezoni na pia wanajipanga kuboresha usikivu wa redio hasa kwenye maeneo ya mipakani.

Alisema wataalamu wote wa Tehama nchini watasajiliwa ili kufahamu wapo wapi na wanafanya nini na kuwajengea uwezo.