Uko hapa: NyumbaniHabari2021 06 03Article 540688

Habari Kuu of Thursday, 3 June 2021

Chanzo: www.habarileo.co.tz

Wizara kukamilisha miradi ‘kichefuchefu’ isaidie umma

Wizara kukamilisha miradi ‘kichefuchefu’ isaidie umma Wizara kukamilisha miradi ‘kichefuchefu’ isaidie umma

WAZIRI wa Maji, Jumaa Aweso, amesema wizara yake ina mkakati wa kukamilisha miradi yote kichefuchefu iliyoshindwa kukamilishwa kwa wakati uliopangiwa, il kuwezesha upatikanaji wa maji kwa wananchi.

Aliyasema hayo wilayani Babati mkoani Manyara alipotembelea mradi wa maji wa Mayoka Minjingu na mradi wa maji Darakuta Magugu na kuzindua Skimu ya Maji Endakiso.

Alisema akiwa naibu waziri wa maji, alitembelea Mradi wa Maji wa Mayoka Minjingu uliopo katika Ziwa Manyara, lakini utekelezaji wa mradi huo haukufanyika licha ya kutengewa zaidi ya Sh bilioni mbili zilizowekwa.

Alisema mageuzi makubwa yamefanyika kuhakikisha wananchi wanapata huduma za maji za uhakika.

"Nawaagiza RUWASA (Wakala ya Usambazaji Maji na Usafi na Mazingira Vijijini ) kufanya kazi usiku na mchana ili kukamilisha miradi hii kwa kuwa sasa hakuna kisingizio cha ukosefu wa fedha wala nguvu kazi; nataka miradi hii ifikapo Juni 30, 2021 iwe imekamilika na nitaizindua," alisema.

Meneja wa RUWASA Mkoa wa Manyara, Wolter Kirita alisema mradi huo ukikamilika utaweza kuzalisha lita 40,000 kwa saa moja ili kutosheleza mahitaji ya wananchi 15,000 wa vijiji vya Kakoi, Minjingu, Nkaiti na Vilima Vitatu.

Akizungumzia Mradi wa Maji wa Darakuta - Magugu unaosimamiwa na Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira mjini Babati (BAWASA), alisema ameridhishwa na ujenzi wa mitambo ya kuchuja ili kuyasafisha maji yatakayowafikia wananchi kuwa maji safi na salama kwa wakazi wa Mji wa Magugu na vijiji jirani kwa kuidhinisha Sh 472,650,432 zilizoombwa kukamilisha mradi huo.

Aidha, Waziri Aweso alizitaka jumuiya za watumia maji katika mradi wa maji aliouzindua wa Skimu ya Maji Endakiso kutunza miundombinu ya maji, kuhifadhi vyanzo vya maji na kuhakikisha fedha zinazopatikana zisaidie kukarabati mabomba chakavu na kukemea ulaji wa fedha hizo.

Mkurugenzi Mtendaji wa Bawasa, Iddy Msuya alibainisha kuwa, fedha hizo zimeombwa kwa ajili ya ununuzi wa dira za maji na kazi ya kukamilisha mradi utakaohudumia wananchi zaidi ya 60,000 wa Kata ya Mwada na Magugu. Mradi huo utakamilika na kuzinduliwa Juni 30, 2020.

Eliza Ole Ngereza, mkazi wa Kijiji cha Endakiso, alisema awali walikuwa wakipata huduma za maji kutoka katika kijiji kilichokuwa kinategemea maji ya chemchem yaliyokuwa yakikauka katikakipindi cha kiangazi na wao kulazimika kutumia maji ya mabwawa.

Join our Newsletter