Uko hapa: NyumbaniHabari2021 09 23Article 559162

Habari za Afya of Thursday, 23 September 2021

Chanzo: www.habarileo.co.tz

Wizara ya Afya kuanza kutumia mfumo wa digital kwenye huduma zake

Mfumo wa kidijiti kuboresha  huduma za afya wazinduliwa Mfumo wa kidijiti kuboresha huduma za afya wazinduliwa

WAZIRI wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk Dorothy Gwajima, amezindua mfumo wa kidijiti wa usimamizi shirikishi katika utoaji wa huduma za afya (AfyaSS), ambao utawezesha upatikanaji wa taarifa sahihi na kwa wakati mwafaka.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa mfumo huo Jijini Dodoma, Dk Gwajima alisema mfumo huo utasaidia kuboresha utoaji wa huduma za afya nchini.

Akielezea namna ya mfumo huo utakavyofanyakazi, Mkuu wa Kitengo kidogo cha Usimamizi Shirikishi kutoka Wizara ya Afya, Dk Chrisogone German, alisema mfumo huo umetengenezwa ili kutatua changamoto mbalimbali zilizopo katika sekta hiyo ikiwemo uratibu kwenye usimamizi na upatikanaji wa taarifa kwa wakati.

Alisema awali ilikuwa ni changamoto sana kumfuatilia mtu lakini sasa mfumo umerahisisha.

"Pia mfumo utasaidia kwenye matumizi ya rasilimali. Kabla ya mfumo huu tulikuwa tunatumia rasilimali nyingi lakini sasa kutakuwa na uratibu mzuri, upatikanaji wa taarifa kutoka kwenye vituo katika ngazi zote utakuwepo na hivyo tutapunguza gharama katika usimamizi," alisema.

Alisema tayari wametoa elimu kwa watu mbalimbali kuanzia ngazi ya taifa hadi wilaya juu ya matumizi ya mfumo huo.

"Ili kurahisisha ufanisi wake wamenunua vishikwambi 900 ambavyo vitagawiwa kwa wadau mbalimbali. Vishikwambi hivi tutavitoa vitatu kwa kila mkoa na kwenye halmashauri pia watapata vitatu," alisema.

Mfumo huo umetengenezwa na Wizara ya Afya kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais Tamisemi na Shirika lisilo la kiserikali la Path kupitia mradi wake wa Data Use Partnership ambao umesaidia kuanzia hatua za awali za utengenezaji wa mfumo tangu mwaka 2017 hadi sasa.