Uko hapa: NyumbaniHabari2021 07 03Article 545089

Habari Kuu of Saturday, 3 July 2021

Chanzo: www.habarileo.co.tz

Wizara ya Mambo ya Nje yavutiwa na kasi ya ujenzi reli ya SGR

Wizara ya Mambo ya Nje yavutiwa na kasi ya ujenzi reli ya SGR Wizara ya Mambo ya Nje yavutiwa na kasi ya ujenzi reli ya SGR

WIZARA ya Mambo ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki inajivunia na kuvutiwa na kasi ya ujenzi wa mradi wa reli mpya ya kisasa (Standard Gauge Railway - SGR) unaoendelea katika hatua mbalimbali nchini.

Haya yameelezwa na Kaimu Mkurugenzi wa Miundombinu ya Uchumi na Huduma za Jamii wa wizara hiyo, Eliabi Chodota alipotembelea mradi huo ambao kwa sasa ndio mradi pekee mkubwa wa reli ya kisasa katika Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Chodota amesema kuwa mradi huo sio tu ni muhimu kwa Tanzania bali utazinufaisha pia nchi wanachama za Jumuiya ya Afrika Mashariki na nchi zingine jirani.

Pia ameeleza kuridhishwa kwake na ushiriki wa raia wa Tanzania katika ujenzi wa mradi huo, ambapo kati ya wafanyakazi zaidi ya 6000, zaidi ya asilimia 80 ni watanzania.

Mradi wa SGR unaotekelezwa kwa awamu tano tofauti kama ifuatavyo: Sehemu ya awamu ya kwanza Kilomita 202 (Dar es Salaam-Morogoro), awamu ya pili Kilomita 348 (Morogoro – Makutopora), awamu ya tatu Kilomita 294 (Makutopora-Tabora), awamu ya nne (Tabora-Isaka), na sehemu ya awamu ya tano kilomita 341 (Isaka-Mwanza).

Aidha mradi huu wa SGR unaoendelea kujengwa kwa kasi, utakapokamilika unatarajiwa kuiunganisha Tanzania na nchi jirani za Rwanda na Uganda, Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).

Sambamba na hayo yote, reli hii mpya inatarajiwa kufanya mapinduzi makubwa katika sekta ya usafiri na usafirishaji nchini kwa kupunguza msongamano barabarani, kupunguza muda wa kusafiri na kupunguza uharibifu wa miundombinu ya barabara.

"Ni wazi kuwa mradi huu utakapokamilika utakapokamilika utapunguza gharama za usafirishaji kwa asilimia 40. Kila treni ya mizigo inatarajiwa kusafirisha hadi tani 10,000 kiasi ambacho kinaweza kusafirishwa na malori 500 kwa njia ya barabara," alieleza kiongozi huyo.

Chodota ametoa rai kwa Watanzania hasa ambao wanazunguka eneo la mradi kuendelea kutoa ushirikiano kwa mamlaka na mkandarasi ili kazi ikamilike kwa wakati.