Uko hapa: NyumbaniHabari2021 06 29Article 544633

Habari Kuu of Tuesday, 29 June 2021

Chanzo: www.habarileo.co.tz

Wizara yapima viwanja 89,000 urais wa Samia

Wizara yapima viwanja 89,000 urais wa Samia Wizara yapima viwanja 89,000 urais wa Samia

WIZARA ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi imepanga na kupima zaidi ya viwanja 89,000 katika halmashauri 24 nchini katika kipindi cha siku 100 za uongozi wa Rais Samia Suluhu.

Aidha, kupitia Programu ya Kupanga, Kupima na Kumilikisha Ardhi (KKK), wizara hiyo imefanya utambuzi wa vipande vya ardhi 40,898 katika halmashauri mbalimbali kwa kutumia njia rahisi na gharama nafuu kwa kutumia wapima wa kati na simu za mkononi.

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi, aliliambia HabariLEO kuhusu ushiriki wa wizara hiyo katika miradi ya kimkakati ya kitaifa kuwa, wizara inaendelea kushiriki utekelezaji wa miradi hiyo kwa kupanga, kupima na kufanya uthamini wa ardhi na mali katika maeneo ya miradi hiyo ukiwamo Mradi wa Ujenzi wa Bwawa la Kuzalisha Umeme la Julius Nyerere, Bomba la Mafuta kutoka Hoima nchini Uganda hadi Chongoleani jijini Tanga, pamoja na ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR).

Kuhusu ujenzi wa bomba la mafuta, Lukuvi alisema: “Katika siku 100, kwa kuzingatia hatua ya kusainiwa kwa mkataba wa uwekezaji baina ya Serikali ya Tanzania na wawekezaji ili kuanza ujenzi wa bomba la mafuta kutoka Hoima, Uganda hadi Chongoleani Tanga, Wizara inaendelea kupima njia ya bomba na kazi itakamilika kabla ya tarehe 30 Juni 2021 (kesho) kupitia ofisi za ardhi za mikoa inayopitiwa na bomba hilo.”

Akizungumzia mradi wa ujenzi wa SGR, Lukuvi alisema wizara hiyo imendelea kuwezesha shughuli mbalimbali za uwekezaji kwa kupanga matumizi mbalimbali katika maeneo mradi.

“Katika kipindi cha Machi hadi Juni, 2021, michoro ya mipangomiji sita imeandaliwa katika kituo cha SGR Morogoro na Kwala,” alisema na kuongeza kuwa, katika michoro viwanja vilivyotengwa kwa ajili ya uwekezaji katika viwanda ni 109 na matumizi mengine.

Aidha, Waziri Lukuvi alisema: “Katika kipindi cha siku 100, wizara kupitia Programu ya Kupanga, Kupima na Kumilikisha ardhi imefanya utambuzi wa vipande vya ardhi 40,898 katika halmashauri za majiji ya Mwanza, Mbeya, Arusha na Manispaa ya Sumbawanga.”

“Kupitia programu hii, Wizara ilifanya utambuzi wa vipande vya ardhi 10,974 katika Jiji la Mwanza, vipande 14,712 jijini Mbeya, vipande 14,252 jijini Arusha na katika Halmashauri ya Manispaa ya Sumbawanga vipande 960,” alisema.