Uko hapa: NyumbaniHabari2021 11 20Article 572950

Habari Kuu of Saturday, 20 November 2021

Chanzo: Nipashe

Yamemkuta! Mchina Anaswa Akichepusha Maji Mto Ruvu

Mchina Anaswa Akichepusha Maji Mto Ruvu Mchina Anaswa Akichepusha Maji Mto Ruvu

IKIWA NI SIKU MOJA baada ya Rais Samia Suluhu Hassan kuwatangazia vita wanaoharibu vyanzo vya maji, mkulima mkubwa raia wa China amenaswa akidaiwa kuchukua maji kutoka Mto Ruvu kwa kutumia mashine yenye uwezo wa kuvuta lita milioni moja.

Raia huyo wa kigeni anayefanya kilimo cha umwagiliaji, amekamatwa na Bodi ya Maji Bonde la Wami/Ruvu katika Kijiji cha Kidogozelo, Chalinze mkoani Pwani.

Ofisa wa Maji Msaidizi wa Bonde hilo, Halima Faraji, alisema jana kuwa mtu huyo alikamatwa katika doria waliyoifanya Novemba 12, mwaka huu baada ya kumbaini mkulima huyo wa mboga kutumia maji ya Mto Ruvu bila kibali. Baada ya kumkamata alitozwa faini ya Sh. milioni tatu.

"Cha kwanza tulimkagua na kubaini hana kibali cha Bodi ya Maji Bonde la Wami/Ruvu kutumia maji ya mto. Tulichukua mashine yake na tukamtaka afike ofisini kwa ajili ya kulipa faini. Novemba 15, akifika ofisini na kulipa faini na tukamzuia kuendelea na umwagiliaji.

“Leo (jana) tena tumefika eneo hili tumekuta kafunga mashine nyingine mpya anaendelea kuvuta maji mtoni," alisema.

Faraji aliongeza kuwa mkulima huyo aliwahi kuomba kibali cha kutumia maji miaka mitano iliyopita lakini hakuwahi kufuatilia na badala yake akawa anaendelea na kilimo cha umwagiliaji katika eneo hilo kinyume cha sheria.

Alisema anachofanya mkulima huyo ni uharibifu mkubwa kwa kuwa anatumia zaidi ya saa nane kuvuta maji kutoka Mto Ruvu kumwagilia, wakati kwa sasa kuna upungufu mkubwa wa maji katika mto huo unaosababisha mgawo wa maji katika mikoa ya Pwani na Dar es Salaam.

"Anachokifanya kina athari kubwa. Moja, hii mashine ameifunga karibu na mto kabisa na kitendo hiki kinachafua maji ya mto kwani mafuta ya dizeli katika mashine yanaingia ndani ya mto na kusababisha uharibifu mkubwa na uchafuzi wa maji. Athari nyingine anatumia maji mengi sana kwani anamwagilia saa nane kwa siku," alisema.

Naye Ofisa Maendeleo ya Jamii wa Bonde hilo, Hhau Sarwatt, alisema baada ya doria za mara kwa mara maji yameongezeka kwenye mto huo.

Alisema kwenye doria hizo, walikuwa wakiendelea kutoa elimu kwa wafugaji na wakulima hili wasiharibu kingo za mto Kwa kuingiza mifugo kwenye mito.