Uko hapa: NyumbaniInfos2019 11 10Article 487315

Sports News of Sunday, 10 November 2019

Chanzo: mwananchi.co.tz

Zahera afunguka siku 571 Yanga

Zahera afunguka siku 571 Yanga

Dar es Salaam. Muda mfupi baada ya Yanga kumtimua Mwinyi Zahera, kocha huyo amefichua namna alivyopambana kuinusuru klabu hiyo katika matukio mbalimbali.

Akizungumza na gazeti hili jana, Zahera alisema katika siku 571 ndani ya Yanga atazikumbuka namna alivyoishi na wachezaji pamoja na wasaidizi wake katika mazingira magumu.

Alisema aliishi nao kama familia moja ili kuhakikisha timu hiyo inafanya vizuri katika mashindano mbalimbali.

“Maisha yangu Yanga yalikuwa na tofauti kubwa, ningeishi kama kocha anavyotakiwa kuishi tusingefanya jambo lolote katika mashindano,” alisema.

“Muda mrefu nilikuwa kama baba wa wachezaji, wasaidizi wangu na hata timu. Kuna changamoto nyingi nililazimika kuzipatia ufumbuzi kuokoa mambo yaende vizuri.”

Kocha huyo alidai aliikuta Yanga katika mtikisiko wa kiuchumi, hivyo alikuwa akitoa fedha zake mfukoni kuwapa wachezaji au wasaidizi wake ili kutatua matatizo ya kifamilia.

Alisema aliamua kutoa fedha hizo kwa kuwa alikuwa na mapenzi na Yanga akitaka wachezaji na benchi la ufundi kuelekeza nguvu katika maandalizi ya mechi za mashindano waliyokuwa wakishiriki.

“Kuna wakati tulikwenda Botswana, baadhi ya viongozi walitangulia mapema, wakati tunafika tukaambiwa tutatumia basi la wapinzani wetu (Township Rollers) tena limeandikwa jina na picha za wachezaji wao ubavuni, unauliza unaambiwa pesa (za kukodi gari) hakuna, nikaamua kuingia mfukoni nikalipa Dola 2000 (Sh4.5 milioni) kukodi basi kwa muda wote,” alisema.

“Tulienda Zambia kucheza na Zesco, watu walitangulia tulipofika wachezaji wakauliza chakula wakaambiwa kipo mara moja saa 11 jioni, nikauliza baada ya hapo, wakasema hakuna chakula, nikasema hapana nikawapeleka wachezaji kula kile cha saa 11 nikawaambia watakula usiku.

“Shida nyingine ikawa uwanja wa mazoezi pesa ya kulipia ikawa hakuna, nikatoa pesa kulipia niliporudi huku nilitafuta taarifa kwa njia yangu nikaambiwa pesa ilitoka lakini kule haikutumika.”

Pia Zahera alidai wakati Yanga ikimaliza kucheza na Pyramids ya Misri walizuiwa hotelini hadi walipie vinywaji na maji ambapo alitoa Sh500,000 ndipo waliporuhusiwa kuondoka.

Makamu Mwenyekiti wa Yanga Frederick Mwakalebela alipotakiwa kutoa ufafanuzi wa madai ya Zahera alisema wanajikita katika maandalizi ya mchezo wa Ligi Kuu dhidi ya Ndanda Ijumaa kwenye Uwanja wa Nangwand.

Join our Newsletter