Uko hapa: NyumbaniHabari2021 11 24Article 573811

Habari Kuu of Wednesday, 24 November 2021

Chanzo: www.tanzaniaweb.com

Zaidi watu 7000 wamekufa kwa ajali ndani ya siku 1460

Zaidi watu 7000 wamekufa kwa ajali ndani ya siku 1460 Zaidi watu 7000 wamekufa kwa ajali ndani ya siku 1460

WATU 7,787 wamefariki dunia katika kipindi cha miaka minne kuanzia mwaka 2018 hadi mwaka huu kutokana na ajali za barabarani.

Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani nchini, Wilbroad Mutafungwa ameyasema hayo jijini Arusha jana kuwa, katika ajali hizo, 13, 429 zilijeruhi watu 14,609.

Alisema hayo wakati akitoa taarifa kwa Rais Samia Suluhu Hassan kwenye uzinduzi wa Wiki ya Nenda kwa Usalama Barabarani 2021 iliyobeba kaulimbiu isemayo ‘Jali maisha yako na ya wengine barabarani.’

Alisema miongoni mwa sababu zinazochangia ajali za barabarani ni makosa ya kibinadamu ukiwamo mwendokasi, uendeshaji wa hatari, ulevi, uzembe wa madereva na watembea kwa miguu, waendesha pikipiki kutokuvaa kofia ngumu, ubovu wa vyombo vya moto, utelezi, vumbi, ukungu na miundombinu ya barabara.

Kwa mujibu wa Kamanda Mutafungwa, mwaka 2018 zilitokea ajali 3,732 ikilinganishwa na ajali 2,704 mwaka 2019 ikiwa ni punguzo la ajali 1,028 sawa na asilimia 27.5.

Alisema idadi ya vifo kwa mwaka 2018 ilikuwa 1,788 ikilinganishwa na vifo 1,440 mwaka 2019 ambapo walifanikiwa kupunguza vifo 348 sawa na asilimia 19.5.

Alisema idadi ya majeruhi kwa mwaka 2018 walikuwa 3,746 ikilinganishwa na majeruhi 2,830 mwaka 2019 ambapo walifanikiwa kupunguza majeruhi 912 sawa na asilimia 24.3.

“Mheshimiwa Rais, mwaka 2019 jumla ya ajali zilizotokea ni 2,704 ikilinganishwa na ajali 1,714 mwaka 2020 na tumefanikiwa kupunguza ajali 990 sawa na asilimia 36.6, wakati vifo kwa mwaka 2019 vilikuwa 1,440 na mwaka 2020 vifo 1,270 na tumefanikiwa kupunguza vifo 170 sawa na asilimia 11.8, huku majeruhi wakiwa 2,830 mwaka 2019 na mwaka 2020 majeruhi ni 2,126 na tumefanikiwa kupunguza majeruhi 708 sawa na asilimia 25.0,” alisema.

Kamanda Mutafungwa alisema katika kipindi cha mwaka jana jumla ya ajali 1,388 zilitokea ikilinganishwa na ajali 1,187 mwaka huu na kupunguza ajali 201 sawa na asilimia 14.5, wakati idadi ya vifo kwa mwaka jana ilikuwa 949 ikilinganishwa na vifo 900 mwaka huu na kupunguza vifo 49 sawa na asilimia 5.2, huku idadi ya majeruhi ilikuwa 1,672 mwaka jana na kwa mwaka huu ni 1,405 hivyo kufanikiwa kupunguza majeruhi 267 sawa na asilimia 16.0.

Kutokana na takwimu hizo, Mutafungwa alimuomba Rais Samia kukiwezesha Kikosi cha Usalama Barabarani vifaa vya kisasa ikiwamo mitambo maalumu ya ukaguzi wa magari ili kukabiliana na ajali, kufunga kamera kwenye barabara kuu za mijini na barabara kuu za nchi.

Mkuu wa Jeshi la Polisi, Simon Sirro alisema makosa ya jinai nchini ikilinganishwa na kipindi cha Januari hadi Septemba mwaka huu, yamepungua kwa asilimia 3.6, wakati makosa ya usalama barabarani yamepungua kwa asilimia 15.4.

Mwenyekiti wa Baraza la Taifa la Usalama Barabarani ambaye ni Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Khamis Hamza Chilo alimuomba Rais Samia wapatiwe sehemu ya mapato yatokanayo na makosa ya usalama barabarani ili wamudu kuendesha shughuli zao kwani baraza hilo halina bajeti.

Ombi hilo lilikataliwa na Rais Samia kwa kuwa nguvu nyingi zitaelekezwa kwenye kutoza faini badala ya kudhibiti makosa ya barabarani.

Hivi karibuni pia ripoti kutoka kwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres zimeeleza kuwa kila sekunde ishirini na nne mtu mmoja anakufa kwenye ajali ya barabarani duniani.

Amesema hayo katika Maadhimisho ya Siku ya Kukumbuka Waliopoteza Maisha au kujeruhiwa kutokana na ajali za barabarani.

Amesema katika kuadhimisha siku hiyo ni wakati wa kutafakari juu ya vifo vilivyosababishwa na ajali za barabarani.

Ameitaka kila nchi, kampuni na raia duniani isaidie juhudi za kitaifa na kimataifa za kuhakikisha barabara zinakuwa salama zaidi hususani kwenye nchi za kipato cha chini na kati ambako zaidi ya asilimia tisini ya vifo vinavyotokana na ajali barabarani hutokea.