Uko hapa: NyumbaniHabari2021 09 20Article 558598

Habari Kuu of Monday, 20 September 2021

Chanzo: TanzaniaWeb

Zawadi Iliyotolewa na IGP Sirro kwa Askari Waliomuua "Gaidi Hamza"

IGP Simon Sirro IGP Simon Sirro

Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini IGP Simon Sirro, ametoa zawadi ikiwemo fedha na vyeti kwa maaskari polisi walioshiriki katika tukio la kupambana na Hamza aliyezua taharuki karibu na zilipo ofisi za ubalozi wa Ufaransa Dar es Salaam Agosti 25 mwaka huu.

Taarifa hiyo imetolewa leo Septemba 20, 2021, na Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Muliro Jumanne Muliro.

“Askari hawa (Waliopambana na Hamza) miongoni mwao walikuwa ni Askari 11, ambao kwa mamlaka za kisheria za uendeshaji wa Jeshi la Polisi Tanzania, IGP amewapa zawadi ya vyeti vya ujasiri na zawadi ya pesa kwa kadri alivyoona inafaa.

“Askari Polisi walipambana kuhakikisha kwamba madhara makubwa zaidi ya yale yaliyotokea hayatokei, nani ambaye hafahamu kama yule mhalifu angeondoka na zile silaha zilizokuwa na magazine 2 na risasi 60 na zingine alizokuwa nazo nini kingefanyika.

“Kama risasi zingepigwa ovyo ovyo na Askari walioenda kupambana pale na jinsi mlivyoona tabia ya wananchi wakisikia matukio wanavyojirundika ni dhahiri kungekuwa na vifo vya wananchi wasiokuwa na hatia.

“Mtu yeyote mwenye taarifa za kweli za majambazi wanaofanya unyang’anyi wa kutumia silaha na taarifa hizo ziwezeshe kukamatwa kwa mhalifu akiwa na silaha ile, Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya DSM, litatoa milioni 2 kwa mtoa taarifa na litatunza siri,” Jumanne Muliro, Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam.