Uko hapa: NyumbaniMichezo2021 06 09Article 541678

Habari za michezo of Wednesday, 9 June 2021

Chanzo: www.habarileo.co.tz

AZAM WATAMBA TUZO ZA VPL

AZAM WATAMBA TUZO ZA VPL AZAM WATAMBA TUZO ZA VPL

MSHAMBULIAJI wa Azam FC, Prince Dube amechaguliwa kuwa Mchezaji Bora wa mwezi Mei wa Ligi Kuu Tanzania Bara (VPL), msimu wa 2020/21 huku George Lwandamina pia wa Azam FC akichaguliwa Kocha Bora wa mwezi huo.

Dube na Lwandamina walitwaa tuzo hiyo baada ya kuwashinda wenzao walioingia nao fainali kwa Mei katika uchambuzi uliofanywa mwishoni mwa wiki iliyopita na Kamati ya Tuzo za VPL, kutokana na mapendekezo ya makocha waliopo viwanja mbalimbali nchini.

Mshambuliaji huyo alikuwa na mchango mkubwa kwa timu yake Mei na kuonesha kiwango cha kuvutia akifunga mabao mawili na kuhusika katika bao moja, ambapo Azam ilicheza michezo miwili na kushinda yote.

Wengine walioingia fainali ni mchezaji wa Kagera Sugar, Erick Mwijage pamoja na kipa wa Yanga, Metacha Mnata, ambao walikuwa na kiwango kizuri kwa mwezi huo.

Hiyo ni mara ya pili kwa Dube kutwaa tuzo hiyo, ambapo mara ya kwanza ilikuwa Septemba mwaka jana, pia Aprili aliingia fainali na kushindwa na kiungo Clatous Chama wa Simba.

Mwingine aliyeingia fainali Aprili alikuwa Raphael Daud wa Ihefu SC.

Gomes

Kwa upande wa Lwandamina, yeye alitwaa tuzo hiyo baada ya kuiongoza Azam kushinda michezo miwili, ambapo ilizifunga KMC mabao 2-1 na Biashara United mabao 2-0 na kuendelea kubaki nafasi ya tatu katika msimamo wa Ligi. Aliwashinda Francis Baraza wa Kagera Sugar na Abdallah Mohamed wa JKT Tanzania.

Wachezaji ambao wametwaa tuzo hiyo kwa msimu huu na miezi yao katika mabano ni Prince Dube (Septemba), Mukoko Tonombe wa Yanga (Oktoba), John Bocco wa Simba (Novemba), Saido Ntibazonkiza wa Yanga (Desemba), Deogratius Mafie wa Biashara United (Januari), Anuary Jabir wa Dodoma Jiji (Februari), Luis Miquissone wa Simba (Machi) na Clatous Chama wa Simba (Aprili).

Makocha waliotwaa tuzo hiyo ni Aristica Cioaba aliyekuwa Azam (Septemba), Cedric Kaze aliyekuwa Yanga (Oktoba), Charles Mkwassa wa Ruvu Shooting (Novemba), Cedrick Kaze, Yanga (Desemba), Francis Baraza aliyekuwa Biashara (Januari), Zuberi Katwila wa Ihefu (Februari), Mohammed Badru wa Gwambina (Machi) na Didier Gomes (Aprili)

Wakati huohuo, Kamati ya Tuzo imemchagua Meneja wa Uwanja wa Azam Complex, Chamazi Dar es Salaam, Sikitu Kilakala, kuwa mshindi wa Tuzo ya Meneja Bora wa Uwanja kwa Mei. Ushindi wa Meneja huyo umefuatia kufanya kwake vizuri katika Menejimenti ya matukio ya michezo iliyofanyika kwenye uwanja huo kwa Mei pamoja na masuala yanayohusu miundombinu uwanjani.