Uko hapa: NyumbaniMichezo2021 11 18Article 572470

Soccer News of Thursday, 18 November 2021

Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz

Ajibu, Sakho wamuumiza kichwa Kocha Simba SC

Ibrahim Ajib Ibrahim Ajib

Bonge la sapraizi. Wachezaji Ibrahim Ajibu na Pape Sakho juzi Jumatatu walimshangaza Kocha wao, Pablo Franco kutokana na viwango vizuri walivyoonyesha kwenye mazoezi ya timu hiyo kwenye Uwanja wa Boko Veterani.

Jina la Ajibu lilikuwa limetoweka miongoni mwa mashabiki wa soka lakini tangu mchezo wa mwisho wa Simba dhidi ya Namungo FC wa ushindi wa bao 1-0 akichangia kwa asilimia kubwa kupatikana kwa bao hilo, amekuwa akitajwa sana na mashabiki hao kwamba ni moto.

Utamu zaidi nyota hao wawili walionyesha kwenye mazoezi hayo juzi na kumkosha kocha Pablo na hivyo ni wazi wataibeba timu.

Hii ina maana ubora wao utasaidia kupunguza mzigo kwa Larry Bwalya ambaye ndiye alikuwa tegemeo akiichezesha timu na kuibeba.

Pablo ambaye amechukua mikoba ya Kocha Didier Gomes ameikuta Simba ikiwa katika kipindi kigumu eneo la kiungo baada ya kuondoka kwa mastaa wawili Clatous Chama na Luis Miquissone.

Hata hivyo, ubora aliouonyesha Ajibu hasa akicheza kama mshambuliaji wa pili (namba 10), akitokea chini.

Alikuwa na ubora kwenye kupeleka mashambulizi huku silaha yake kubwa ikiwa ni uhakika wake kwenye kupiga pasi za mwisho kwa washambuliaji jambo lililomfanya Pablo awe na furaha muda wake asiamini anachokiona.

Kwa upande wa kiraka Pape Sakho, amerejea kwa kasi na ameonekana kuwa na kasi kwenye kupandisha mashambulizi na bora katika kupunguza mabeki.

Alionyesha ufundi wa kupiga mashuti akiwa nje ya boksi jambo liliwavutia benchi la ufundi na mashabiki. Pia utulivu awapo na mpira na kupokea pasi kisha kuingia ndani ya boksi ni mambo yaliyomvutia Pablo na wakati wote alionekana kutabasamu.

Nyota mwingine aliyemkosha Kocha Pablo ni Yusuph Mhilu kutokana na umakini wake wa kukokota mipira na kupiga krosi za uhakika kutokea upande wa kushoto.

HITIMANA AFUNGUKA

Kocha msaidizi wa Simba, Thiery Hitimana alisema urejeo wa Sakho kikosini ni jambo zuri kwa sababu kutaongeza kitu eneo la ushambuliaji.

Alisema mchezaji huyo alikuwa anasumbuliwa na maumivu na kukosa mechi ya kirafiki, lakini kwa namna alivyomwona mazoezini anaamini suala la kucheza lipo kwa kocha mkuu (Pablo).

“Sakho ni mchezaji mwenye faida mbili, anaweza kucheza kama kiungo pia mshambuliaji wa pili. Ni jambo zuri amerejea na kocha mkuu ndio atajua kama atamtumia mchezo ujao au vipi,” alisem Hitimana.

Wachezaji wengine waliokuwepo katika mazoezi hayo ni Jeremiah Kisubi, Ally Salim, Shomari Kapombe, Mohamed Hussein, Mzamiru Yassin, Erasto Nyoni, John Bocco, Israel Patrick, Gadiel Michael, Yusuph Mhilu, Kennedy Juma, Erick Inonga na Pascal Wawa.

Wengine ni Hassan Dilunga, Meddie Kagere, Ibrahimu Ajibu, Duncan Nyoni, Bernard Morrison, Abdulswamad Kassim, Jimson Mwanuke na wachezaji wengine kutoka timu ya vijana.

Simba itashuka dimbani kwenye mchezo wa raundi ya sita wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Ruvu Shooting, Novemba 19, kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, jijini Mwanza.