Uko hapa: NyumbaniMichezo2021 08 16Article 551746

Soccer News of Monday, 16 August 2021

Chanzo: Mwanaspoti

Azam, Simba, Yanga zapewa mchongo

Sehemu ya Kikosi cha Wachezaji wa Yanga Sehemu ya Kikosi cha Wachezaji wa Yanga

Wawakilishi wa Tanzania, Simba, Yanga, Azam na Biashara United zimechorewa ramani ya kuweza kutoboa kwenye mechi zao za kimataifa za msimu huu zinazoandaliwa na Shirikisho la Soka Afrika (CAF).

Simba na Yanga zitashiriki Ligi ya Mabingwa Afrika, huku Azam na Biashara zitaiwakilisha nchi kwenye Kombe la Shirikisho Afrika na wadau wa soka baada ya kuichungulia ratiba zao kwenye michuano hiyo ya CAF, wamezishauri zianze kuwasoma wapinzani wao sasa kujua aina ya soka lao kabla ya kukabiliana nao.

Yanga imepangwa kucheza na River United, ikianzia nyumbani kabla ya kumalizia ugenini, huku Simba itaanzia ugenini katika mechi ya raundi ya kwanza dhidi ya mshindi kati ya Jwaneng ya Botswana au DFC Beme ya Afrika ya Kati na iwapo Yanga itapenya itavaana na Fasil Kenema au Al Hilal.

Azam itacheza na Horseed Sports ya Somalia nq ikivuka hapo itakwaruzana na Pyramid ya Misri, huku Biashara ikivaana na FC Dikhil ya Djibouti na Mwenyekiti wa zamani wa Simba, Aden Rage, alisema ratiba ya timu zinazoshiriki michuano ya Caf, zina ugumu na uwepesi ni kitendo cha kujipanga ili wafike mbali.

“Yanga wanatakiwa kuisoma vyema River United, kutokana na kuwa na kituo cha soka, hivyo wanaweza wakatumia asilimia kubwa ya wachezaji wao, japo imeanzishwa 2016, Azam naona mechi ya kwanza itakuwa rahisi ila ya pili ngumu, vivyo hivyo kwa Simba,” amesema Rage na kuongeza;

Naye Katibu wa Mwadui FC, Joseph Mbogo Dabu amezishauri timu hizo zianze kuwasoma watakaokutana nazo ili wajue mbinu za kukabiliana nazo mapema. “Ratiba yake ina ugumu na wepesi, lakini kila kitu lazima ujipange na kuangalia ni mbinu zitakazowabeba.”

Staa wa zamani wa Yanga, Idd Moshi amesema kinachotakiwa siyo kuangalia ratiba tena bali zifanye maandalizi ya maana, huku wasajili wachezaji watakaoendana na thamani ya michuano hiyo.

Mtendaji Mkuu wa Azam, Abdulkarim Amin ‘Popat’ amesema wamejiandaa vizuri kwenye michuano hiyo mikubwa Afrika licha ya kutambua ugumu kwenye michuano hiyo ila malengo yao makubwa yakiwa ni kufika hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika (CC).

WASIKIE MAKOCHA

Kocha wa KMC, Habib Kondo amesema “Simba, Yanga, Azam na Biashara United, zitumie muda wa kutafuta undani wa timu hizo, zifanye maandalizi yakuwafikisha mbali, pamoja na kuheshimu kila hatua,” amesema.

Naye Kocha wa Mtibwa Sugar, Mohamed Badru amesema timu zinazokwenda kushiriki lazima zijue zinakwenda kukutana na mpira wa sampuli gani, ndipo zitaweza kupiga hatua.

“Mfano mzuri ni Simba ipo ya kimataifa unaona inacheza mpira tofauti na ule unaoonyeshwa kwenye ligi ya ndani, vivyo hivyo Yanga, Azam FC na Biashara United ziige mfano huo,” amesema.