Uko hapa: NyumbaniMichezo2021 08 18Article 552124

Soccer News of Wednesday, 18 August 2021

Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz

Azam yashtukia janja ya Waarabu

Mshambuliaji wa Azam FC, Prince Dube Mshambuliaji wa Azam FC, Prince Dube

Azam FC kwenye Kombe la Shirikisho wanaanza na Horseed ya Somalia wakivuka hapo wanakwaana na Pyramids ya Misri. Sasa Pyramids hao hao wameleta Sh 1.8 bilioni mezani wanamtaka Prince Dube.

Viongozi wamewachomolea na kuwasisitiza kwamba; “Kijana hauzwi.” Akizungumza kuhusiana na sakata hilo, Mtendaji Mkuu wa Azam FC, Abdulkarim Nurdin ‘Popat’ alisema ni kweli wamepokea ofa zaidi ya mbili lakini kwa upande wao hawapo tayari kufanya biashara ya mchezaji yeyote.

Amesema msimu huu matarajio yao ni kufanya vizuri katika mashindano ya ndani na Kimataifa hivyo mipango ya kocha na wao kama kiongozi ni kutengeneza timu itakayokaa pamoja muda mrefu.

“Hatutaki kurudia makosa, tunahitaji timu itakayokaa pamoja muda mrefu ili kuwa na ushindani ndani na nje, kumbuka tunatarajia kuiwakilisha nchi kwenye mashindano ya kimataifa Kombe la Shirikisho Afrika,” amesema.

Popat ameongeza kuwa malengo ni kufanya vizuri na sio kuzuia wachezaji kwenda kujaribu changamoto kwenye timu nyingine muda wa kufanya hivyo ukifika watafanyahivyo lakini kwa msimu huu hawana nafasi ya kuuza mtu yeyote.

“Tuna ofa nyingi sio hiyo moja lakini hatuna mpango wowote wa kufanya biashara ya mchezaji na ndio maana tumefanya usajili wa nyota wengi, lengo ni kufanya vizuri na sio kufanya biashara,” amesema.

Dube aliyejiunga na Azam FC msimu ulioisha kwa mkataba wa mwaka mmoja akitokea Highlanders FC ya Bulawayo Zambia amehusika kwenye mabao 19 akifunga 14 na kutoa asisti tano na ataendelea kuitumikia timu hiyo baada ya kuongeza mkataba wa miaka miwili.

Katika hatua nyingine, ili kuendana na mabadiliko ya soko yanayotokea kila siku, jana Azam ilimtambulisha Jonas Tiboroha kuwa mkurugenzi wa michezo huku ikijinasibu kufanya mambo yao kimya kimya.

Cheo hicho hapo awali hakikuwa na mtu ndani ya klabu hiyo na Azam imekuwa ya kwanza kutangaza wadhifa huo ambao hakuna timu nyingine Tanzania yenye mkurugenzi wa michezo.

Kazi yake ni kusimamia masuala yote yanayohusu mpira ndani ya klabu - cheo ambacho ni cha pili kwa ukubwa baada ya ofisa mtendaji mkuu wa klabu na vingine vinafuata ikiwemo mkurugenzi wa ufundi.