Uko hapa: NyumbaniMichezo2021 08 15Article 551614

Soccer News of Sunday, 15 August 2021

Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz

Bangala afunga hesabu Yanga, atangulia kambini

Sehemu ya kikosi cha Yanga wakiwa uwanja wa ndege kuelekea Morocco Sehemu ya kikosi cha Yanga wakiwa uwanja wa ndege kuelekea Morocco

Yanga imepaa zao kwenda Morocco kuweka kambi, mabosi wa klabu hiyo wamekamilisha hesabu zao za usajili kwa kumsainisha juu kwa juu beki kisiki Yannick Bangala Litombo na ndiye atakayekuwa mchezaji wa kwanza kutua kambini kwa maandalizi ya msimu mpya.

Lakini Bangala akifunga hesabu hizo kwa kusaini mkataba wa miaka miwili, utamu ni amekuwa mchezaji wa kwanza pia kupokewa kwa hati yake ya uhamisho (ITC) kutoka klabu yake ya FAR Rabat ya Morocco, winga Jesus Moloko ameanika siri ambazo ni kama sumu kwa timu pinzania zitakazokutana na Yanga katika Ligi Kuu Bara, Kombe la Shirikisho (ASFC) na Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu.

Tuanze na usajili huu, Yanga imemalizana na Bangala aliyeondoka FAR Rabat inayonolewa na kocha wa zamani wa Simba, Sven VanderBroeck kwa kuvunja mkataba wake kwa makubaliano ya pande mbili na leo atakuwa mtu wa kwanza kutua kambini kwao wakati wowote.

Bangala anatua Yanga kuja kuziba nafasi ya nahodha wao wa zamani, Lamine Moro aliyevunja mkataba na timu hiyo wiki chache baada ya ligi kumalizika msimu uliopita.

Yanga inaondoka leo saa tisa alasiri na msafara wa wachezaji 28 wakiwemo beki Djuma Shaban, Jesus Moloko, Fiston Mayele na Heritier Makambo kujiandaa na mbio za ligi msimu ujao wakifungua na mchezo wa Ligi ya Mabingwa dhidi ya Rivers United ya Nigeria.

Safari ya Yanga ya siku zisizopungua 10 itayoanza leo mchana wakipitia Dubai kisha kesho kutua Casablanca mchana utaongozwa na Makamu Mwenyekiti wa Yanga Frederick Mwakalebela na Makamu Mwenyekiti wa kamati ya mashindano ya timu hiyo Mhandisi Hersi Said.

Moloko afichua

Winga mpya wa timu hiyo Jesus Moloko jana amefichua kuwa urahisi wa kazi yake ndani ya Yanga ni hatua ya mabosi wa timu hiyo kuwapa ajira mastraika wawili Fiston Mayele na Heritier Makambo.

Moloko anayetua Yanga kuziba nafasi ya Tuisila Kisinda aliyeuzwa Morocco kwa klabu ya RS Berkane alisema haitakuwa ngumu kufanya vizuri kwake kwa kuwa anaungana na Mayele ambaye alikuwa naye AS Vita na anamjua aina ya mipira anayotaka na alihusika katika mabao 8 kati ya 13 aliyofunga Mayele msimu uliopita.

“Namjua Mayele anataka mipira ya aina gani, kunileta hapa pamoja na yeye ni kama viongozi wamerahisisha kazi zetu. Naamini watu watafurahi sana,” amesema Moloko.

“Makambo sijawahi kucheza naye lakini nimeuliza kwa makocha na hata wenzangu wananiambia ni mshambuliaji bora anayejua kufunga hii sasa kama tutafanya kazi vizuri Yanga itakuwa na safu nzuri ya ushambuliaji na hapo bado kuna wachezaji wengine tuliowakuta ambao nao tutashirikiana kwa pamoja.”