Uko hapa: NyumbaniMichezo2021 09 22Article 559012

Habari za michezo of Wednesday, 22 September 2021

Chanzo: globalpublishers.co.tz

Barbara: TP Mazembe ni Kipimo Sahihi

Barbara: TP Mazembe ni Kipimo Sahihi Barbara: TP Mazembe ni Kipimo Sahihi

MTENDAJI Mkuu wa Simba, Barbara Gonzalez, amefunguka kuwa, kama wangetaka kushinda kirahisi mchezo wa kilele cha Tamasha la Simba Day, basi wangeialika timu dhaifu, huku akitamba kuwa mchezo wao dhidi ya TP Mazembe ni kipimo tosha kuelekea mtanange wa Ngao ya Jamii dhidi ya Yanga.

Simba ilikubali kipigo cha bao 1-0 dhidi ya TP Mazembe kwenye mchezo wa kimataifa wa kirafiki uliochezwa Jumapili, Uwanja wa Mkapa, Dar ambapo bao pekee la TP Mazembe liliwekwa kimiani na Jean Beleke dakika ya 85.

Akizungumza na Spoti Xtra mara baada ya mchezo huo, Barbara alifunguka kwamba: “Kwanza kabisa niwashukuru mashabiki na wanachama wa Simba kwa kujitokeza kwa wingi, hii imedhihirisha ukubwa wa klabu yetu.

“Kuhusu kupoteza mchezo wetu dhidi ya TP Mazembe hiyo ni sehemu ya mchezo na TP Mazembe ndiyo kipimo sahihi kwetu kuona ni wapi kuna mapungufu ili tuweze kuboresha.

“Tungehitaji ushindi kirahisi tungeweza kuialika timu dhaifu na tungepata ushindi mkubwa, hivyo mchezo huu ni kipimo tosha kuelekea mchezo wetu wa tarehe 25 dhidi ya Yanga ambao ninaamini tutafanya vizuri.”

Kikosi cha Simba, kimerejea kambini kuanza maandalizi kuelekea mchezo wa Ngao ya Jamii dhidi ya Yanga unaotarajiwa kupigwa Septemba 25, mwaka huu katika Dimba la Mkapa, Dar, huku Simba wakiwa na kumbukumbu ya kutwaa taji hilo kwa misimu minne mfululizo.