Uko hapa: NyumbaniMichezo2021 08 15Article 551575

Habari za michezo of Sunday, 15 August 2021

Chanzo: www.habarileo.co.tz

Bashungwa: Fuateni nyayo za Azam

Bashungwa: Fuateni nyayo za Azam Bashungwa: Fuateni nyayo za Azam

SERIKALI imesema ilitamani kuona klabu zote zinazoshiriki Ligi Kuu Soka Tanzania Bara, zinafuata nyayo za Azam FC kwa kuwa na vituo vya kukuza soka la vijana.

Akizungumza Dar es Salaam jana katika uzinduzi wa nembo mpya ya Azam FC, Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Innocent Bashungwa alisema fedha zitakazonufaisha klabu hizo zisaidie kukuza vijana ili baadaye wawe hazina kwenye timu za wakubwa.

“Suala hili niwaachie Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) na wadau tuangalie namna gani kuandaa vipaji, sehemu ya fedha kama tulivyozungumza na Rais wa Shirikisho la Soka Afrika (Caf) Patrick Motsepe zinufaishe klabu kuanzisha vituo vya soka kusaidia kuleta tija,”alisema.

Kuhusu nembo alisema ni muhimu kwa maendeleo ya timu ya Azam na mchezo wa mpira wa miguu huku akisema serikali ina imani na kampuni za Azam kutokana na mchango mkubwa katika sekta ya michezo.

Alizungumzia pia, umuhimu wa klabu hiyo kuanzisha klabu ya soka ya wanawake ili kukuza vipaji.

Mwenyekiti wa Kamati ya Huduma na Maendeleo ya Jamii ya Bunge Stanslaus Nyongo alisema, wamefurahishwa na hatua hiyo ya kuzindua nembo mpya na kwamba Azam FC imekuwa chachu ya maendeleo ya soka nchini.

“Azam FC mmekuwa ni mfano kwa klabu nyingine zote Tanzania, tunapenda kusema igeni Azam FC inachofanya, hatusikii watu kubabaika kwamba hawalipwi mishahara, mnaendesha vizuri kila klabu ni vizuri ikaiga ili kufanya mpira wa soka usonge mbele,”

Alisema ndoto ya kamati hiyo ni kuona mpira unatengeneza ajira kwa watanzania na kwenda kuitangaza nchi kimataifa.

Ofisa Mtendaji Mkuu wa Azam FC Abdulkarim Amin ‘Popat’ alisema awali kuwa uzinduzi wa nembo hiyo utawajengea taswira na kuwapa matumaini mapya kuelekea msimu mpya wa Ligi Kuu.

Alisema malengo yao ni kuhakikisha wanafanya vizuri katika michuano ya kimataifa ikiwezekana kufikia hatua ya makundi na

mbele zaidi.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa TFF, Kidao Wilfred alisema shirikisho hilo litaendelea kuunga mkono klabu mbalimbali ikiwemo Azam FC iliyojipambanua kwenye mfumo bora wa uendeshaji kwenye kiwango cha kimataifa.

“Kila wakati tunapotembelewa na wageni wetu kutoka vyama vya michezo vya kimataifa kama Uefa, Fifa na Caf, Azam FC imekuwa ni mfano bora wa klabu inayoendeshwa kwa uwekezaji bora barani Afrika na kutupa heshima kubwa kama nchi,”alisema.