Uko hapa: NyumbaniMichezo2021 08 23Article 553216

Soccer News of Monday, 23 August 2021

Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz

Biashara yaanza kujifua Nyamagana, Kocha azungumzia wapinzani CAF

Kikosi cha Biashara United Kikosi cha Biashara United

Timu ya Biashara United Mara imeweka kambi yake jijini Mwanza kwa ajili ya maandalizi ya msimu mpya ikiwemo michuano ya kimataifa, ambapo leo wameanza kujifua katika uwanja wa Nyamagana.

Timu hiyo iko kwenye maandalizi ya mchezo wa kombe la Shirikisho barani Afrika dhidi ya FC Dikhil ya Djibouti utakaochezwa kati ya Septemba 10 na 12 pamoja na Ligi Kuu itakayoanza Septemba 29, mwaka huu.

Mazoezi ya wanajeshi hao wa mpakani yameanza saa 4:15 asubuhi hadi saa 6:50 mchana chini ya Kocha Mkuu, Patrick Okumu yakijikita zaidi kwenye kufunga mabao, kupiga pasi, kutengeneza nafasi na kupiga krosi.

Pia katika mazoezi hayo baadhi ya nyota wapya wa kikosi hicho akiwemo mshambuliaji mpya Kassim Mdoe na Atupele Green na beki Boniphace Maganga walipasha na wenzao, huku nahodha Abdulmajid Mangalo, kipa Daniel Mgore na winga mpya kutoka Kenya, Tayo Mathew wakikosekana.

Kocha Mkuu, Patrick Okumu ameiambia Mwanaspoti Digital kuwa  watajifua uwanjani hapo kwa siku tatu na wameamua kuweka kambi jijini Mwanza ili kuzoea mazingira baada ya kuuchagua  uwanja wa CCM Kirumba kama uwanja wao wa nyumbani kwa ajili ya mechi za kimataifa.

Amesema kambi hiyo itawasaidia kupata utulivu, kurejesha utimamu wa mwili na  kutengeneza mfumo na mbinu kwa ajili ya msimu mpya.

Akiwazungumzia wapinzani wao FC Dikhil ya Djibouti kwenye kombe la shirikisho Afrika, Okumu amesema kuwa wanatarajia itakuwa mechi ngumu kwani kila timu iliyopata nafasi kwenye michuano hiyo imestahili na imejiandaa hivyo hawatachukulia poa watajiandaa kutoa upinzani wa kweli.

Amesema bado wachezaji sita akiwemo nahodha Mangalo ambaye amepewa mapumziko, Tayo Mathew anayemalizia mechi za ligi Kenya na Daniel Mgore ambaye alihudhuria hafla ya kukabidhi kombe kwa timu ya taifa chini ya miaka 23 wataripoti kambini hivi karibuni.